Na Abdu Madenge - WMJJWM, DODOMA
Serikali imesema, umefika wakati kwa kushirikiana na wadau kubuni mbinu na mikakati mbadala na za haraka kuja na afua za kisayansi zitakazowezesha kukabiliana na Malezi Duni ndani ya Jamii.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amoni Mpanju wakati akifungua Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Malezi na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, Julai 13, 2023 Jijini Dodoma.
Mpanju amesema ukosefu wa elimu sahihi ya malezi na makuzi kwa wazazi na walezi hasa kwa watoto wa kiume ni miongoni mwa sababu zinazochochea mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa watoto na vijana nchini.
Mpanju amesema ipo haja kwa wazazi na walezi kuja na mfumo mzuri wa malezi wenye kushinikiza uwajibikaji wa baba na mama katika kuboresha malezi na ulinzi wa watoto.
"Kwa mujibu wa Taarifa ya Makosa ya Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji za Jeshi la Polisi kwa watoto kwenye kipindi cha Januari hadi Disemba, 2022 kulikuwa na matukio 12,163 (Wavulana 2,201 na Wasichana 9,962 nchini. Matukio yaliyoongoza ni Ubakaji (6,335), ulawiti (1,557) na Mimba za utotoni matukio (1,555).amesema Mpanju na kuongeza
"Serikali inathamini sana watoto kwa kutambua ndiyo rasilimali muhimu kwa ujenzi wa Taifa, hivyo imekuwa ikichukua hatua za makusudi kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kukuza maadili kwenye familia na jamii" Amefafanua Mpanju.
Wakati wa kikao hicho Mpanju amesema tayari Serikali imeandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 inayohimiza kuimarishwa kwa Haki za kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa, Sera ya Elimu na Mafunzo inayohimiza elimu bure kwa kila mtoto kutoka shule za msingi hadi sekondari; Sheria ya Mtoto Sura ya 13 inatoa ulinzi kwa mtoto, Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ikiwa ni jitihada za kumlea na kumkuza Mtoto wa Kitanzania.
Akitoa Maelezo ya utangulizi Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Mtoto Sebastian Kitiku amesema, jamii inahitaji tafiti za mara kwa mara ili kujua maeneo ambayo yanatakiwa kutiliwa mkazo kwenye masuala ya malezi na makuzi ya Mtoto yanayozingatia shahidi na afua za kisayansi
"Changamoto ya malezi wote tunazifahamu linda mtoto wako asiathirike kimwili na kisaikolojia dhidi ya sababu zinazoleta hali hiyo, ikiwa ni pamoja na maendeleo katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano," amesema Kitiku.
Akizungumza kwa niaba ya ISC, NIMRI na vyuo vikuu vya Oxford na CapeTown Mkurugenzi wa ICS Tanzania Kudely Sokoine amesema wamesheshirikiana kwa pamoja kuekeleza ajenda hiyo na mpango wa kujenga mazingira wezeshi ya kisera ili kuongeza na kupanua wigo wa utekelezaji wa Afua za malezi unaozingatia ushahidi wa kisayansi ili kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto
"Malengo Mahususi na Maalum ya mpango huu nikufanya upembuzi kuangalia sera za Tanzania katika masuala ya malezi, aidhaa tumejaribu pia kuangalua afua zinazotekelezwa na wadau, Mpango huu unaunga mkono jitihada za Viongozi wa Tanzia akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wadau wengine."amesema Kudely
Mkutano huo wa siku moja, umewaleta kwa pamoja wadau kutoka Serikalini na asasi za kiraiya pamoja na wadau wa Maendeleo.
No comments:
Post a Comment