Na Okuly Julius -Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge amesema Ili kukuza uwekezaji katika shughuli za usafiri majini na uvuvi, Serikali ya Awamu ya 6 kupitia TASAC inaendelea kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport- MLVMCT ).
Lengo la Mradi huo ni kushughulikia changamoto za usafiri majini, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri majini na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria.
Bw. Mkeyenge ameyasema hayo Leo Julai 27,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TASAC kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Amesema mradi huo unatekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda umepangwa kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za Mradi ni Shilingi bilioni 19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani (national activities) na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda (regional activities) zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda.
"Mradi huu unatarajiwa kukamilika mnano mwezi Disemba, 2024 na tayari Mkandarasi ameshakabidhiwa maeneo ya kufanyia kazi katika mradi huu na Hadi sasa, Mkandarasi ameshaanza ujenzi kwa vituo vidogo vya Mara-Musoma, Kanyala na Nansio-Ukerewe" Ameeleza Bw. Mkeyenge
Aidha mpango mkakati wa utekelezaji katika mwaka wa fedha 2023/24 Bw. Mkeyenge amesema itasaidia uboreshaji na udhibiti wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji nchini sambamba na kuweka ushindani ili kuhakikisha huduma za usafiri majini zinakuwa endelevu.
Kuratibu maandalizi ya Amri, kutoa maoni na kuwezesha uandaaji rasimu za Kanuni na nyenzo za utendaji zitoazo mwongozo kuhusu udhibiti huduma za usafiri majini, usalama na ulinzi kwa vyombo vya usafiri majini na uchafuzi baharini kutoka katika meli.
Pamoja na hayo amesema kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 Shirika litasimamia utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu Usafirishaji kwa njia ya Maji inayoratibiwa na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organization).
" lingine ni Kushirikisha wadau katika kufanya mapitio na marekebisho ya Sheria na Kanuni mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania, sura 415". Amesema
"Napenda kuchukua nafasi hii kwa heshima kubwa kuishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha TASAC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kusimamia Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport- MLVMCT)". Ameshukuru Bw. Mkeyenge
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari - Maelezo, Gerson Msigwa amesema Serikali inataka kushirikiana na sekta binafsi kuendesha Bandari, mikataba na watakaoendesha bado haijasainiwa.
"Sasa hivi ndio wataalamu wako mezani kuzungumza kuhusu mikataba, muda na gharama lakini hakuna Bandari iliyouzwa, wataalamu watakapokamilisha majadiliano tutaangalia maslahi yetu yako wapi na maoni yanayotolewa na Watanzania yatazingatia". Amesema Msigwa
Amesema Serikali iko macho wakati wote kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa.
No comments:
Post a Comment