WAZAZI NA WALEZI WAHIMIZWA KUTOWAFICHA WATOTO WENYE ULEMAVU. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 31, 2023

WAZAZI NA WALEZI WAHIMIZWA KUTOWAFICHA WATOTO WENYE ULEMAVU.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga (wa kwanza kushoto) akizungumza wakati wa ziara yake alipotembelea wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwanga Viziwi Mkoani Kilimanjaro (kulia) ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya.
Baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa kutosikia katika Shule ya Msingi Viziwi pamoja na washiriki wengine wakifuatilia matukio mbalimbali katika kikao kilichofanyika Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga (wa pili kushoto) akishiriki chakula cha pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwanga Viziwi Mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro Mhe. Abdallah Mwaipaya (aliyesimama) akifafanua jambo wakati za ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipowasili katika Wilaya hiyo kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwanga Viziwi Mkoani Kilimanjaro.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga Mhe. Joseph Tadayo akieleza jambo wakati wa ziara hiyo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)


Na Mwandishi wetu- Kilimanjaro

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kutowaficha watoto wao ndani akisema kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao za msingi.


Mhe. Ummy ametoa kauli hiyo katika ziara yake alipotembelea wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwanga Viziwi, Wilaya ya Same pamoja na Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).


Amesema kuwa watu wenye ulemavu wana haki sawa na watu wengine hivyo inapaswa kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja na fursa ili waweze kujikwamua kiuchumi na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.


“Watu wenye ulemavu msivunjike moyo, watoto mlioko hapa viziwi msikate tamaa mna uwezo wa kusoma mkafika mbali, mna uwezo wa kufanya shughuli yoyote kwa sababu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo kwa ajili yenu amewezesha elimu bure kwahiyo tutumie nafasi hiyo,”Amesema Mhe. Ummy.


Pia amewahimiza watu wenye ulemavu kutojinyanyapaa na kujiona hawafai akisema wana haki sawa na watu wengine hivyo jamii inatakiwa kuwatambua na kuwapa kipaumbele katika huduma mbalimbali na hata fursa za ajira.


Aidha Mhe. Ummy ametoa mitungi ya gesi ya kupikia 93 kwa watu wenye ulemavu Wilaya ya Mwanga kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni hatua ya uhifadhi wa mazingira na kuepuka madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya kuni.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro Mhe. Abdallah Mwaipaya ameishukuru Serikali kwa kuanzisha shule za watu wenye ulemavu kwani hutoa fursa kwao kupata ujuzi na stadi za maisha ambazo husaidia kundi hilo kujitambua na kujua nafasi yao katika jamii.


“Wilaya yetu ni moja ya Wilaya chache zenye shule hizi ambazo zinawajenga katika stadi za maisha kulingana na hali ya ulemavu wao hatimaye kukabiliana na hali waliyo nayo kwa sababu kuwa mtu mwenye ulemavu haina maana hauwezi hivyo uwepo wa shule hizi ni hatua muhimu sana,”Ameeleza Mhe. Mwaipaya.


Aidha Akitoa taarifa ya Watu Wenye Ulemavu Katibu wa Shirikisho la Vya vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro Bwa. Jeremia Shayo amebainisha kwamba wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa viungo bandia, wakalimani wa lugha ya alama katika baadhi ya Taasisi hali ambayo hukwamisha mawasiliano pindi wanapofika mahali husika kupata huduma.

No comments:

Post a Comment