Na Okuly Julius -Dodoma
Vishoka ni watu ambao wapo nje ya mfumo na wamekuwa wakiwasababishia watanzania hasara kutokana na kuwafungia umeme kinyume na utaratibu na pengine kutokidhi vigezo vibavyotakiwa kitaalamu
Mhandisi Hassan Saidy ametoa wito huo Leo Agosti 18,2023 Jijini Dodoma, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo na mwelekeo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
"Vishoka wanagharima sana kutokana na kufanya kazi nje ya utaratibu na hapa Wananchi ndipo wanatakiwa kujifunza kuwa ni vyema kuwatumia Wataalamu kama wanataka kuunganishiwa umeme kuepukana na hasara zinazozuilika,"amesema Mhandisi Saidy
Pia amewataka wananchi kutumia umeme uliopo Kwa shughuli za uzalishaji na sio kuishia kuwasha taa na Tv Kwani gharama za kufikisha umeme ni kubwa hivyo ni vyema wananchi wakautumia Kwa matumizi mingine.
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI
Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II)
Mradi huo unahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 vilivyobaki kati ya vijiji vyote 12,318 pamoja na kujenga njia za umeme wa Msongo wa Kati zenye urefu wa kilomita 23,526, kujenga njia za umeme wa Msongo Mdogo zenye urefu wa kilomita 12,159, kufunga mashineumba 4,071 na kuunganisha wateja wa awali wapatao 258,660.
Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa kiasi cha Shilingi trilioni 1.58. Mradi huu kwa sasa upo katika hatua ya utekelezaji ambapo unatarajiwa kukamilika Disemba 2023 kwa mikataba 32 na Juni 2024 kwa mikataba saba (7). Utekelezaji wa mradi kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 73.
Mradi wa Kusambaza Umeme katika Vitongoji – (Hamlet Electrification Project – HEP)
Baada ya kukamilika kwa mradi wa Kupeleka Umeme katika Vijiji, Serikali imepanga kufikisha umeme katika vitongoji ili kuhakikisha kuwa umeme unafika na kutumika maeneo ya vijijini Tanzania Bara.
Mhandisi Saidy amesema serikali kupitia REA ilifanya utambuzi wa wigo wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara na kubaini kuwa vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na miundombinu ya umeme nchini ni 36,101 kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo Tanzania Bara. Aidha, gharama za kufikisha miundombinu ya umeme katika vitongoji hivyo (36,101) ni Shilingi trilioni 6.7
"Serikali ilipata mkopo wa gharama nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kupitia dirisha la Extended Credit Facility ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 100 zitatumika kuanza utekelezaji wa mradi huu katika vitongoji 654 katika mikoa ya Songwe na Kigoma na hivyo kufanya vitongoji ambavyo havina umeme kuwa 36,101,"amesema Mhandisi Saidy
UFAFANUZI JUU YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA VIJIJINI
Mradi wa Usambazaji wa Mitungi ya Gesi ya Kupikia (LPG)
Wakala umeanza kutekeleza Mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000 yenye thamani ya shilingi bilioni 3 pamoja na majiko banifu 200,000 (laki mbili) katika maeneo ya vijijini;
Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 Jumla ya fedha takribani TZS bilioni 10 zimetengwa kwaajili ya kufanikisha mradi huo.
Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia (CNG)
Kusambaza gesi asilia ya kupikia katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani (Pembezoni mwa Mkuza wa Bomba Kuu la Kusafirisha Gesi Asilia);
Utekelezaji wa Mradi huu utahusisha REA na TPDC;
Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 Jumla ya TZS bilion 20 zinatarajiwa kutumika;
Mradi huu utahusisha ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia (CNG) lenye urefu wa km 44.4 (Mnazi Mmoja – Lindi (km 22.9) na Mkuranga – Pwani (km 21.5)),Jumla ya nyumba/wateja 980 kunufaisha (Mnazi Mmoja – Lindi, wateja 451 na Mkuranga-Pwani, wateja 529);
Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Utaratibu wa Malipo kwa Matokeo (RBF)
Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) imetenga Dola za Kimarekani (USD Milioni 6) kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia;
Takribani Majiko 200,000 yanatarajiwa kusambazwa katika maeneo mbali mbali ya vijijini na vijiji miji (Peri Urban) Tanzania bara;
Wanufaikaji: Wazalishaiji na Wasambazaji Wadogo wa Ndani wa majiko banifu;
Lengo: Kukuza na kuboresha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia;
Kwa sasa, Wakala upo kwenye mchakato wa uandaaji wa taratibu na kanuni za utoaji wa ruzuku hizo.
MRADI WA KUWEZESHA UJENZI WA VITUO VIDOGO VYA KUSAMBAZA BIDHAA ZA PETROLI VIJIJINI KWA NJIA YA MKOPO NAFUU (CREDIT LINE FACILITY)
Mhandisi Saidy amesema kuwa Mradi huo unahusu kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za mafuta katika maeneo mbalimbali ya vijijini.
Mradi wa utoaji Mikopo ya Ujenzi na Uendeshaji wa Vituo Vidogo vya mafuta ya Petroli na Diseli vijijini Tanzania bara ambapo kiasi cha Mwisho cha Mkopo ni TZS 75,000,000,Kiasi cha Riba ni 5%,Muda wa Marejesho ni Miaka 7.
Ambapo katika mwaka 2023/24 kiasi cha TZS bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu kwa waendelezaji.
Kwasasa, Wakala unaendelea kupokea Maombi ya Waombaji na Mwisho wa Kupokea Maombi ni 25 Agosti 2023.
Malengo Makuu ikiwa ni:
Kulinda Mazingira na Afya ya Watumiaji na Kuboresha upatikanaji na Usambazaji wa Mafuta vijijini.
Wakala wa Nishati Vijijini umeendelea kuhamasisha na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini katika maeneo mbalimbali katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment