Na Mwandishi wetu -Dodoma
WASAMBAJI wa mbolea nchini, wameipongeza Mamlaka ya Udhibiti ya Mbolea nchini (TFRA), kwa kuboresha mfumo wa kidijitali wa uuzaji mbolea ya ruzuku kwa wakulima hapa nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walipotembelea banda la TFRA, kwenye maonesho ya Nanenane Kanda Kati, yanayoendelea katika uwanja wa Nzuguni Jijini Dodoma, wakala Abdul Baswa wa kampuni ya Agri-Baswa ya mjini Songea, amesema msimu huu wakulima watarajie kupata mbolea kwa wakati kutokana na kwamba mfumo wa utoaji mbolea meboreshwa na serikali.
"Tunaishukuru sana TFRA kutokana na moboresho waliyoyafanya kwenye mfumo wa utoaji mbolea ya ruzuku, tunaomba waendelee kuboresha zaidi ikiwemo kutoa elimu kwa wakulima ili wajitokeze kwa wingi kujisajili," Baswa alikazia.
Kwa upande wake Pius Nzege, kutoka Tanzania Education Published LTD, amesema kutokana na mfumo wa utoaji mbolea ulivyoboreshwa, anatarajia kujisajili kwa ajili ya kupata sifa za kuwa wakala wa mbolea kwa msimu ujao wa kilimo.
Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora wa Mbolea kutoka TFRA, Aziz Mtambo amewataka mawakala kujitokeza kwa wingi kuchukua mbolea kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Amesema hivi sasa mfumo wa utoaji mbolea umeboreshwa kwa kiasi kikubwa hivyo hakutakuwa na changamoto yoyote kwenye mfumo wa utoaji mbolea ya ruzuku.
Naye Afisa Udhibiti Ubora wa TFRA Steven Gossi amewataka wakulima kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kujisajili ili waweze kunufaika na mbolea ya Ruzuku.
Amesema TFRA inaendelea kutoa elimu ya namna ya kujisajili, ili uweze kuingia katika mfumo ambao utakuwezesha kupata mbolea ya Ruzuku.
No comments:
Post a Comment