MAAFISA USTAWI WA JAMII WATAKIWA KUENDELEA KUTOA ELIMU YA AFYA YA AKILI KWA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 6, 2023

MAAFISA USTAWI WA JAMII WATAKIWA KUENDELEA KUTOA ELIMU YA AFYA YA AKILI KWA JAMII


Na Okuly Julius-Dodoma

Maafisa Ustawi wa Jamii kote nchini,wametakiwa kuendelea kutoa elimu ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa jamii ili kupunguza au kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye makundi mbalimbali ya kijamii.


Maelekezo hayo yametolewa Leo Septemba 6,2023,Jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii Tanzania Kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt.Philip Mpango

Ambapo ,Dkt.Biteko amesema kutokana na ushahidi unaoonesha kuwa afya duni ya akili huchangia vitendo vya ukatili.


Pia amewataka Maafisa Ustawi hoa ,kuendelea kusuluhisha migogoro kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii na Ofisi za Ustawi wa Jamii ngazi za Halmashauri nchini. Nimefahamishwa kwamba katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023, jumla ya mashauri 28,773 yalipokelewa na kati ya hayo 22,844 yalifanyiwa usuluhishi katika Mabaraza ya Usuluhishi na Ofisi za Ustawi wa Jamii na 5,929 yalipewa rufaa kwenda mahamakani.


Pia ameielekeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuendelea kuwatambua na kuwapatia huduma watoto walio katika mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na huduma za chakula, malazi, mavazi, elimu, matibabu na lishe.


"Nimejulishwa kuwa migogoro ya ndoa ilipungua kwa 27% katika kipindi hicho kutokana na jitihada zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali. Pamoja na matokeo hayo mazuri, nasisitiza zaidi kuendelea kusuluhisha migogoro ya ndoa na kuipatia ufumbuzi haraka ili kutoathiri zaidi familia na ustawi wa jamii yetu,


Na kuongeza kuwa "Nimefahamishwa kuwa jumla ya watoto 335,971 (Me 168,634, Ke 167,337) walio katika mazingira hatarishi wametambuliwa na kupatiwa huduma katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Aprili 2023. Miongoni mwa hao, watoto 26,000 waliotelekezwa, manusura wa vitendo vya ukatili, wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu na wanaoishi kwenye makao ya watoto wameunganishwa na familia zao ili kuwahakikishia malezi, matunzo na ulinzi. Naipongeza Wizara kwa jitihada hizo, na naelekeza kuongeza juhudi zaidi kuwatambua watoto wa kundi hili na kaya zao na kuchukua hatua stahiki za kuwanusuru kulingana na tathmini ya mazingira yao,"amesema Dkt.Biteko


Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya jamii, jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema maafisa wamekuwa wakitoa huduma kwa kuzingatia Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali ya Serikali kwa kushirikisha Wadau lakini bado kuna Changamoto kubwa ya upungufu mkubwa wa Maafisa hawa takribani 20,057 kwa sasa sawa na asilimia 95.3 ya wanaotakiwa kuanzia ngazi ya mkoa mpaka ngazi ya Kijiji/Mtaa.


Naye mwenyekiti wa Maafisa ustawi wa jamii Mkoa Martin Chuwa amesema changamoto ya kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili, ongezeko la mmonyoko wa maadili, migogoro katika ndoa ,migogoro ya familia hupelekea ongezeko la watoto wa mitaani.
Aidha ameiomba wizara na taaisis zinazohusika kuajiri maafisa ustawi kila mwaka ili kupunguza upungufu uliopo.



Mkutano huu umeenda sambamba na Uzinduzi wa kuazimisha Miaka 50 ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Uzinduzi wa Wiki ya Ustawi wa Jamii pamoja na Uzinduzi wa Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa 2023; Mwongozo wa Mafunzo ya Uwiano wa Kijinsia na Ujumuishwaji Jamii katika Huduma za Ustawi wa Jamii 2022, na Kiongozi cha Taifa cha Uelimishaji wa Huduma za Ustawi wa Jamii na Majukumu ya Viongozi.

Kauli mbiu katika Mkutano wa Maafisa ustawi wa jamii ni “Malezi, makuzi kwa afya bora ya akili ni jukumu letu sote”.



No comments:

Post a Comment