Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS) kwa kushirikiana Wizara ya Afya na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), zinaendelea kutekeleza mradi wa Afua Jumuishi (Total Facility Approach) unaolenga kuondoa unyanyapaa na ubaguzi miongoni mwa watoa huduma za afya kwa wagonjwa wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na watumiaji wa dawa za kulevya.
Kikao cha siku tano kinafanyika mkoani Morogoro, kikilenga kuandaa nyenzo za kufundishia ili kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi wa vyuo vya kati, juu ya unyanyapaa na ubaguzi.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Chuo cha MUCOHAS, Dkt. Bonny Betson, amesema mradi huo umejikita katika kuboresha uelewa, mitazamo na ujuzi wa watoa huduma ili kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa ni jumuishi, rafiki na zenye kuzingatia utu wa kila mteja.
“Huu ni mwaka wa tatu tangu tulipoanza mradi huu, na kwa sasa tumetekeleza awamu ya kwanza hapa MUCOHAS kwa wanafunzi na walimu, baada ya hapo tunapitia mtaala mdogo tulioutengeneza mahsusi kwa ajili ya kuendesha mafunzo haya,” amesema Dkt. Betson.
Ameongeza kuwa kabla ya kuandaa mtaala huo, utafiti wa awali ulifanyika kwa wanafunzi na walimu waliopata mafunzo ili kubaini mahitaji halisi na changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma na matokeo ya utafiti huo yalitumika kutengeneza mtaala unaolenga kutumika pia katika vyuo vingine vya afya nchini, ikiwa ni hatua muhimu ya kupunguza unyanyapaa na ubaguzi miongoni mwa watoa huduma za afya.
Utekelezaji wa mradi wa Afua Jumuishi unaendana na malengo ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hususan katika kuondoa unyanyapaa unaodhorotesha upatikanaji na utumiaji wa huduma kwa watu wanaoishi na VVU Pamoja na watumiaji wa madawa ya kulevya.
Hili litachangia katika mikakati ya Serikali iliyowekwa ili kutokomeza maambukizi ya VVU ifikapo mwaka 2030, kwa kuimarisha utoaji wa huduma rafiki, jumuishi na zenye usawa kwa wote.




No comments:
Post a Comment