GRIDI YA TAIFA YA MAJI NA UTEKELEZAJI WAKE NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 28, 2026

GRIDI YA TAIFA YA MAJI NA UTEKELEZAJI WAKE NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali ya Awamu ya Sita imeanza utekelezaji wa Mradi wa Mtandao wa Taifa wa Kusambaza Maji (National Water Grid) unaolenga kutoa maji kutoka vyanzo vya uhakika kama maziwa na mito mikubwa na kuyasambaza kwenda maeneo yenye uhaba wa maji nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kupitia Ziwa Victoria, miradi ya maji katika mikoa ya Musoma, Rorya–Tarime, Bunda, Simiyu, Mwanza, Geita, Chato, Biharamulo na Bukoba inaendelea kutekelezwa, huku mingine ikiwa tayari imeanza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, usanifu wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida (LVD Project) umekamilika na taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea.

Kwa upande wa Ziwa Tanganyika, Serikali imepata mtaalam mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi itakayohudumia mikoa ya Kigoma, Katavi, Songwe na Rukwa. Hatua za awali pia zinaendelea kwa miradi ya Ziwa Nyasa kwa lengo la kuhudumia mikoa ya Njombe na Ruvuma. Vilevile, usanifu wa miradi ya kutumia maji ya mito mikubwa ya Rufiji na Ruvuma umekamilika, hatua inayofungua fursa kubwa ya kuimarisha upatikanaji wa maji katika mikoa ya Kusini na Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 28, 2026 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais Samia, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia uimarishaji wa huduma za msingi, hususan sekta ya maji, mijini na vijijini.

Waziri Aweso amesema kuwa ndani ya kipindi cha siku 100, Wizara ya Maji imechukua hatua mbalimbali za kimkakati ikiwemo ununuzi wa dira za maji za malipo kabla (prepaid meters) 2,271 ambazo zinaendelea kufungwa kwa wateja katika maeneo mbalimbali nchini. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi katika matumizi ya maji, kudhibiti upotevu wa mapato na kuhakikisha wateja wanapata huduma kulingana na matumizi halisi.

Ameeleza kuwa ujenzi wa mabwawa ya ukubwa wa kati ya Gidahababieg, Mwambazi na Mwamashindike unaendelea kwa kasi, ambapo mabwawa hayo yanatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya mita za ujazo 1,457,000 za maji na kunufaisha wananchi zaidi ya 1,817,800 pamoja na mifugo zaidi ya 356,400.

“Kukamilika kwa miradi hii kutachangia kuimarisha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya kijamii na kiuchumi, hususan katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya upungufu wa maji,” amesema Waziri Aweso.

Aidha, Serikali imeimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji kupitia upandaji wa miti zaidi ya 705,300 katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kulinda mazingira na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika kuimarisha usimamizi wa miradi ya maji vijijini, Serikali imenunua na kugawa pikipiki 216 kwa Jumuiya za Watoa Huduma za Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs). Vilevile, jumla ya shilingi bilioni 198.84 zimelipwa kwa wakandarasi na wataalam washauri wanaotekeleza miradi ya maji nchini, hali iliyoharakisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Serikali pia imelipa fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maji, imechimba visima 151 katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na kupata hati safi za miradi mikubwa baada ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), jambo linaloonesha uwajibikaji na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma.

Katika kipindi cha siku 100, jumla ya miradi 16 ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 16.28 imekamilika katika mikoa ya Simiyu, Njombe, Iringa, Kilimanjaro, Dodoma, Geita na Tanga, na kuwezesha wananchi zaidi ya 118,400 kupata huduma ya maji safi na salama.

Wizara inaendelea kutekeleza miradi 71 ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 142.8, ambapo baadhi yake tayari imeanza kutoa huduma. Miradi hiyo inatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 2,887,029 ikiwemo miradi ya Maboresho ya Miundombinu ya Maji Mtwara Mjini, Mradi wa Nzuguni Awamu ya Kwanza Dodoma, Mradi wa Kigamboni Lot III Dar es Salaam pamoja na Mradi wa Mkinga–Horohoro mkoani Tanga unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 57,000.

Aidha, Serikali imelipa malipo ya awali ya shilingi bilioni 5.99 kwa Mradi wa Maji wa Tunduma wenye thamani ya shilingi bilioni 119. Vilevile, mikataba ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji na usafi wa mazingira katika miji ya Morogoro na Mwanza imesainiwa, sambamba na mikataba mingine mitano ya miradi ya maji katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Geita, Singida na Simiyu.

Mafanikio haya ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanaakisi dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha huduma za maji zinaboreshwa, rasilimali za maji zinalindwa na maendeleo endelevu yanapatikana kwa manufaa ya wananchi wote.



No comments:

Post a Comment