Matokeo ya Sensa Chachu ya Maendeleo - Makinda - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 23, 2023

Matokeo ya Sensa Chachu ya Maendeleo - Makinda


Na Mwandishi wetu - Kigoma

Waandishi wa habari wameaswa kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 kuwawezesha wananchi kujiletea maendelea katika ngazi zote.

Hayo yamesemwa na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 Mhe. Anne Semamba Makinda wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa Septemba 22 mjini Kigoma.

Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuwawezesha wananchi kutumia takwimu hizi za matokeo ya Sensa kujiletea maendelea, kusaidia viongozi katika ngazi zote katika kupanga mipango ya maendeleo", alisisitiza mhe. Makinda.

Akifafanua amesema waandishi wa habari wamefanya kazi kubwa ya Kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye Sensa mwaka 2022 hivyo kwa sasa jukumu kubwa ni kuwawezesha wananchi kutumia takwimu kujenga uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Sanjari na hilo, amewaasa kuzingatia kuwa takwimu hizo ni msingi wa mabadiliko ya jamii hivyo jukumu lao ni kuwawezesha wananchi kuyafikia.

Mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Kigoma Katavi na Rukwa yanafanyika kwa siku mbili mjini Kigoma yakishirikisha waandishi 70 kutoka katika mikoa hiyo. 

Mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na uchambuzi wa takwimu za Sensa kwa ajili ya habari, Usambazaji wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 kidigitali, Wajibu wa vyombo vya habari katika kusambaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, Majukumu ya NBS, Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa ramani na Mwongozo wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022.

No comments:

Post a Comment