Na Gideon Gregory, Dodoma.
Tanzania imeungana na mataifa mbalimbali ulimwenguni kama Mwanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya Mtoto wa Kike Kimataifa iliyoongozwa na kauli mbiu isemayo “Wakati ni sasa haki ni Maisha yetu”.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Oktoba 11,2023 jijini Dodoma katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato na mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ambapo amesema kuwa idadi ya wasichana waliorejea shuleni kupitia mfumo rasmi na ambao sio rasmi baada ya kukatisha masomo yao kutokana na changamoto mbalimbali imeongezeka kwa mwaka 2022/23.
“Idadi ya wasichana waliorejea shuleni kupitia mfumo rasmi na usio rasmi imeongezeka mpaka sasa na hadi kufikia 7995 kwa mwaka 2022/23, wanafunzi 676 waliofaulu vizuri kwa masomo ya sayansi wakiwemo wanafunzi wa kike 261 ambapo ni sawa na 41% ya wanafunzi ambao walionufaika na Samia Scoral ship,”amesema Prof. Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda amesema kuwa kulingana na changamoto wanazozipitia watoto wenye mahitaji maalumu nchini watoe taarifa katika Ofisi ya wizara ya elimu ili waweze kutatuliwa changamoto na kutimiza ndoto zao.
“Watoto wenye mahitaji maalumu wenye changamoto ya kusoma watoe taarifa katika Ofisi za Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunawasaidia kwasababu hayo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kazi yetu sisi ni kutekeleza maelekezo yake na tunayatekeleza kwa raha kwasababu ni maelekezo mazuri mno,”amesema Prof. Mkenda.
Amesema uwepo wa Mazingira wezeshi umewezesha watoto wenye mahitaji maalumu kupata elimu na hivyo kuhakikisha kila mtoto na kila mwananchi anapata elimu hiyo sawa na watu wote wanavyopata.
Naye mwakilishi wa Naibu katibu mkuu Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Susan Nusu amesema kuwa Ofisi hiyo inasisitiza kwa hali na mali watu wote kuanzia ngazi ya kaya na mamlaka zote za serikali Tanzania bara kuhakikisha wanawalinda wototo wote wanakuwa katika mazingira salama.
“Tunasisitiza kwa hali na mali viongozi wote kuanzia ngazi ya kaya, mtaa, kijiji, kata wilaya na mamlaka zote zilizopo katika Mikoa yote ya Tanzania bara kuhakikisha mtoto wa kike si anarejeshwa shuleni tu lakini anakuwa katika Mazingira salama, anakuwa katika mikono salama ya watanzania wote wanao mzunguka,”amesema.
Nao baadhi ya wasichana waliorejea shuleni wamempongeza Rais Samia kwa kutoa nafasi ya wao kurejea shuleni ili waweze kutimiza ndoto zao na kuwaasa wale walioko shuleni kuhakikisha wanakuwa chachu ya kuwasaidia wenzao wanaopitia changamoto mbalimbali katika jamii.
No comments:
Post a Comment