KAMATI YARIDHISHWA NA KASI YA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI NZUGUNI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 27, 2023

KAMATI YARIDHISHWA NA KASI YA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI NZUGUNI


Na Okuly Julius - Dodoma 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imefanya ziara leo Oktoba 27,2023 ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa visima vya maji Nzuguni jijini Dodoma unaogharimu kiasi Cha Shilingi bilioni 4.8 na kuridhishwa na Maendeleo ya Ujenzi wake.

Akizungumza katika Ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Jackson Kiswaga amesema kuwa Ziara hiyo ililenga kukagua na kujionea utekelezaji wa maelekezo ya Kamati hiyo ya kutaka Wizara ya Maji kutafuta Mradi wa Muda mfupi wa kuhakikisha wananchi wanapata maji kabla ya kukamilika Kwa Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria ambao unatarajiwa kuwa suluhisho la upungufu wa maji katika Jiji la Dodoma. 

Hivyo ametoa maelekezo Kwa Wizara ya  Maji na DUWASA kuongeza Kasi ya utekelezaji wa Mradi huo ili kuhakikisha wananchi wanapata Maji Kwa wakati uliyokusudiwa.

Kamati hiyo, 
 imepongeza juhudi za Serikali kwa kuchukua hatua na kutoa fedha ili kupunguza uhaba wa huduma ya maji katika jiji la Dodoma ambapo kuna upungufu wa lita milioni 65, lita milioni 68 ndio zinazozalishwa hivi sasa.

Hivi sasa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) inachimba kisima kikubwa cha mita 300 ili kuongeza wingi wa maji kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Kamati hiyo imepata Fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Kituo Mahiri cha Rasilimali za Maji ,unaofanyika katika eneo la Kolon jijini Dodoma.


Ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga amepongeza juhudi zilizofanyika katika ujenzi wa kituo hicho na kusisitiza kitumike kuwakusanya wataalamu mbalimbali wa rasilimali za maji kutoka kona zote za Dunia ili kuisaidia nchi katika uendelezaji wa rasilimali za maji.

Kwa upande wake ,Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema kituo hicho kitakapokamilika Pamoja na kazi nyingine, kitatumika katika masuala ya utafiti wa rasilimali za maji.

Amesema ujenzi wake umefika asilimia 75 na inatarajiwa kitakamilika mapema mwaka 2024 na eneo la ujenzi wa kituo hicho limetumika katika masuala ya utafiti wa maji chini ya ardhi kabla ya uhuru, tangu mwaka 1956.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema mradi wa maji wa Nzuguni utekelezaji wake umefika asilimia 93 na ndani ya saa 24 wananchi wataona mabadiliko ya huduma ya maji kupitia mradi huo.

Mradi huo wa Maji Nzuguni ukikamilika utakuwa unazalisha maji lita Milioni 7 Kwa siku na utahudumia Wananchi zaidi ya 75,000 katika Kata ya Nzuguni ,Ilazo ,Kisasa Nyumba 300 na maeneo mengine ya Jirani


No comments:

Post a Comment