WAMILIKI WA SHULE BINAFSI NI WATU MUHIMU NCHINI: PROF. MKENDA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, October 10, 2023

WAMILIKI WA SHULE BINAFSI NI WATU MUHIMU NCHINI: PROF. MKENDA.


Na Gideon Gregory, Dodoma.

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa wamiliki wa shule binafsi ni watu muhimu na wanahitajika pakubwa nchini jambo ambalo limepelekea serikali kupiga hatua katika kufaulisha wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi ambapo takribani 20% ya wahitimu ndiyo wanaobakia mtaani.

Waziri Mkenda ameyasema hayo leo Oktoba 10,2023 Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Wizara hiyo na wamiliki wa shule zisizo za serikali.


“Labda niseme jambo moja muhimu, nyie ni wadau muhimu sana zamani tulikuwa tunaona mabasi yanapishana kwenda nje ya nchi wanafunzi wanaenda kusoma lakini baada ya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu na kuruhusu watu binafsi kuanza kumiliki shule imeweza kutusaidia pakubwa kwa hilo nawapongeza”,amesema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa kwa sasa mfumo wa elimu nchini umebadilika ambapo umri wa mtoto kuanza shule utakuwa ni kuanzia miaka sita na mtoto atapaswa kumaliza shule akiwa na miaka 13 na ikitokea akaacha shule atarudishwa ili aweze kumalizia elimu yake.

Aidha amesema wataenda kuanzisha masomo ya amali na wanafunzi watakaosoma mafunzo hayo na kumaliza kidato cha nne watapata vyeti kutoka NACTVET.

“Kama mapendekezo yatapita leo kuanzia darasa la 3 wataanza na mtaala mpya, kidato cha nne na tano wataanza na mtaala mpya pamoja na vyuo vya ualimu mwaka wa kwanza lengo la kufanya haya yote ni kutaka kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini,”amesema Prof. Mkenda.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi naibu waziri elimu sayansi na teknolojia Mhe. Omary Kipanga amesema
kuwa wanaamini kikao hicho kitaleta tija kwa wamiliki wa shule pamoja na taifa kwa ujumla.

Naye Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema kuwa ofisi yao ina wajibu wa kuwaandaa vyema vijana kwa kushirikiana na taasisi binafsi kwani huko ndipo wanapopatikana wafanyabiashara wazuri watakao lisaidia taifa .

Pia amesema suala la malezi na makuzi limekuwa suala mtambuka hivyo wasimamizi wa shule wanapaswa kulisimamia vyema suala hilo na kuangalia namna ya kuwekeza na kuwasaidia vijana maana serikali inawategemea sana wamiliki hao wa shule katika kuwaandaa kwa maisha yajayo.

“Naomba pia muangalie namna ya kufanya pale mnapotoa nafasi za kazi kuweza kutoa na nafasi za walemavu na matarajio kama sisi serikali ni kutengeneza usawa katika kila sekta hapa nchi,”amesema Katambi.


No comments:

Post a Comment