UDSM KUADHIMISHA WIKI YA UTAFITI NA UBUNIFU KUANZIA JUNI 9 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 8, 2026

UDSM KUADHIMISHA WIKI YA UTAFITI NA UBUNIFU KUANZIA JUNI 9

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yatakayofanyika kuanzia Juni 9 hadi 11, 2026, yakilenga kuonesha mchango wa utafiti na ubunifu katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Juni 8, 2026 Jijini Dar es Salaam Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - Utafiti, Prof. Nelson Boniface amesema maadhimisho hayo yatabeba kaulimbiu isemayo, “Kutumia Utajiri wa Madini Yaliyopo Nchini Tanzania katika Kukuza Nishati Jadidifu, Mageuzi ya Kidijitali na Usalama wa Jamii.” 

Hafla ya ufunguzi itafanyika katika Ukumbi wa Huruma huku maonyesho yakifanyika katika viwanja vya Maktaba Mpya ya chuo hicho.

Ameeleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inaendana na juhudi za taifa za kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo, huku ikisisitiza umuhimu wa madini ya kimkakati kama grafiti, nikeli, lithiamu, kobalti, urani na shaba katika kukuza nishati jadidifu na mageuzi ya kidijitali.

"Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za madini ambao ukiongezewa thamani kupitia utafiti, ubunifu na teknolojia unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)". Amesema

Amesema kuwa maadhimisho hayo yatahusisha mihadhara ya kitaaluma, makongamano, mijadala ya kitaalamu, maonyesho ya tafiti na ubunifu pamoja na majukwaa ya kujenga ushirikiano kati ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi, viwanda na serikali.

Pamoja na hayo amesema kuwa katika siku ya ufunguzi Juni 9, mhadhara wa wazi utatolewa na Rais wa Singapore mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, ambaye anatarajiwa kuwa nchini kwa ziara ya kikazi. 

Mhadhara huo unalenga kutoa fursa kwa wanafunzi, watafiti, wasomi na wadau mbalimbali kujifunza uzoefu wa Singapore katika maendeleo, uongozi na ubunifu.

Aidha, amesema kuwa Juni 10 kutafanyika majadiliano maalum ya ushirikiano wa kimkakati yatakayowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kujadili namna ya kuharakisha matumizi ya matokeo ya tafiti, kuongeza thamani ya madini na kuimarisha mchango wa sayansi na teknolojia katika maendeleo ya taifa.

Maadhimisho hayo yatafungwa Juni 11 chini ya mgeni rasmi Prof. Carolyne Nombo, huku wananchi, wanafunzi, watafiti, wabunifu na wadau wa maendeleo wakihimizwa kushiriki katika shughuli zote zitakazokuwa wazi kwa umma kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni kila siku.

No comments:

Post a Comment