Na, mwandishi wetu – Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeingia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa maafa nchini kwa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu.
Akizungumza mapema hii leo (08 Juni, 2026) katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Dkt. Jim Yonazi, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga mifumo madhubuti ya kiutendaji inayoongozwa na maarifa, sayansi na teknolojia ikiwemo matumizi ya Akili Unde (AI) katika kukabiliana na maafa.
Amesema makubaliano hayo yanatekeleza pia mapendekezo ya Mkutano wa Nane wa Umoja wa Mataifa wa Jukwaa la Dunia la Upunguzaji wa Vihatarishi vya Maafa uliofanyika Geneva, Uswisi, mwezi Juni 2025, na yanaashiria mabadiliko ya kimkakati katika namna Serikali inavyoshughulikia changamoto za maafa kutoka mfumo wa kusubiri majanga hadi mfumo wa kujikita katika kinga, maandalizi na tahadhari.
“Vyuo vikuu na taasisi za utafiti, ikiwemo Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, zina jukumu muhimu la kuzalisha maarifa na suluhisho za kisayansi zitakazosaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa nchini,”amesema.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa makubaliano hayo, Serikali itaandaa Mpango Kazi wa utekelezaji pamoja na Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Usimamizi wa Maafa itakayobainisha maeneo ya kipaumbele yanayohitaji ufumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia.
Dkt. Yonazi amesisitiza kuwa mafanikio ya makubaliano hayo yatapimwa kwa matokeo halisi yatakayochangia kuongeza usalama wa wananchi, kulinda rasilimali za taifa na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya maafa.
Ushirikiano huo unaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoweka msisitizo katika matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Prof.Preksedis Marco Ndomba amesema kuwa taasisi imeandika historia kwa kusaini hati ya ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo ameeleza kuwa mchakato huu ulianza muda mrefu na matunda yake yameanza kuonekana jambo ambalo ni mafanikio makubwa.
“Tunaahidi juu ya kufanikisha makubaliano hayo kwa kuwa, uwezo huo tunao, utalaam upo wa kutosha kwa kushirikiana kwenye masuala ya viatarishi kitaifa ili kufanikisha adhima hii ya Serikali,” Alisema Profesa Ndomba.






No comments:
Post a Comment