WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUTOFANYA KAZI KWA MAZOEA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, October 22, 2023

WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUTOFANYA KAZI KWA MAZOEA

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mhandisi, Juma Mdeke ( wakwanza kulia) akizungumza wakati wa kikao na wadau wa Tasnia ya mbolea ikiwa ni pamoja na wakurugenzi wa wilaya, Makatibu Tawala, Maafisa Ugani, Maafisa Tawala, kampuni na mawakala wa mbolea wa mkoani Ruvuma tarehe 21 Oktoba, 2023
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, (TFRA) Dkt. Anthony Diallo, akizungumza baada ya kumtembelewa ofisini kwake akiwa ameambatana na wajumbe wa bodi na menejimenti ya TFRA, tarehe 21 Oktoba, 2023
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na kampuni za mbolea na mawakala wa mbolea wa Mkoa wa Ruvuma mara baada ya kuhitimisha kikao baina ya uongozi wa TFRA na wadau wa Tasnia ya Mbolea mkoani Ruvuma tarehe 21 Oktoba, 2023
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Shimo Peter Shimo ( wa kwanza kulia) akizungumza jambo wakati wa kikao na wadau wa Tasnia ya Mbolea ikiwa ni pamoja na wakurugenzi wa Wilaya, Makatibu Tawala, Maafisa Ugani, Maafisa Tawala, wawakilishi wa kampuni na mawakala wa mbolea wa Mkoa wa Ruvuma tarehe 21 Oktoba, 2023. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt. Anthony Diallo, katikati mjumbe wa bodi hiyo, Mhandisi Juma Mdeke

Na Mwandishi wetu - Ruvuma 

Imeelezwa kuwa, utendaji kazi wa mazoea unaofanywa na watumishi wa umma unasababishwa na kutokuwajibishwa kwa kutokuwa na matokeo katika nafasi zao.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ndani ya mkoa wa Ruvuma.

Akihoji kwa mifano, viongozi wa ngazi mbalimbali aliokutana nao wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Songea na kwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru , Dkt. Diallo alitaka kujua endapo kuna kiongozi yeyote aliyeomba kupewa taarifa ya upimaji wa afya ya udongo kwa maafisa ugani waliokabidhiwa vifaa vya kupima na kubaini afya ya udongo katika maeneo yao.

Aidha, alihoji endapo yupo kiongozi yeyote katika ngazi ya Mkoa au Wilaya aliyechukua hatua ya kuhakiki taarifa za usajili zilizotolewa na wakulima kwa ajili ya kunufaika na mbolea ya ruzuku?

Mara baada ya kubaini mambo hayo kutokufanyika Dkt. Diallo aliwashauri viongozi hao kufanya hivyo na kuwawezesha maafisa wao kuhakiki taarifa za wakulima ili mbolea inayotolewa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inawanufaisha watanzania na si vinginevyo.

Aidha, Dkt. Diallo ameshauri kuwa, kutokana na hali ya kuwa na mvua nyingi katika Mkoa wa Ruvuma, ni dhahiri eneo hilo linaadhiriwa na hali ya mmomonyoko wa udongo na kushauri wakulima kulima kilimo cha kontua na pia kupima afya ya udongo mara kwa mara ili kujua hali ya udongo wao.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni za mbolea mkoani Ruvuma, Ayubu Njogela, amesema kampuni za mbolea zimejipanga kuhakikisha mbolea zinafikishwa kila mahala na kwa wakati.

Ameishukuru Mamlaka kwa kuhakikisha mawakala na vyama vya ushirika vimesajiliwa na kupata namba za uwakala na kuwaeleza wakulima kuwa mbolea zipo na zitasambazwa kulingana na mahitaji na bei zitauzwa kulingana na umbali.

Akifunga kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Mwankoh amekiri kupokea maoni na ushauri wa Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA na kuahidi kufanyia kazi.

No comments:

Post a Comment