Na Mwandishi wetu,Tanga
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea Vituo viwili vya Uzalishaji Umeme vya Hale na New Pangani Falls, na kujiridhisha na maendeleo ya ukarabati wa vituo hivyo.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. David Mathayo imetembelea vituo hivyo tarehe 14 Novemba 2023, vilivyopo wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Hadi sasa vituo hivyo vimeweza kuongeza hali ya uzalishaji na upatikanaji wa huduma ya umeme kwa kuzalisha Megawati 68 kituo cha Pangani na Megawati 10.5 katika kituo cha Hale.
Akizungumza mara baada ya kutembelea Vituo hivyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. David Mathayo, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha kuzalisha umeme cha Hale ambao utasaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme nchini ifikapo Aprili 2024.
*"Nipende kuwajulisha Wananchi kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameendelea na jitihada zake za kuhakikisha kwamba nchi inakuwa na umeme wa kutosha na ametoa shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha kuzalisha Umeme cha Hale,"* amesema Dkt. Mathayo
Aliwataka Wakandarasi na Wizara ya Nishati kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kukamilisha miradi inayoendelea ifikapo mwaka 2025 ili nchi isiwe na changamoto ya mgao wa Nishati hiyo muhimu katika Uchumi wa Taifa.
"Nichukue nafasi hii kuwahimiza Wakandarasi na Wizara ya Nishati mhakikishe Miradi ya umeme nchini inafanya kazi ili kutimiza ndoto za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nchi inakuwa na Umeme wa uhakika muda wote "Amesisitiza Dkt. Mathayo
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka amesema jukumu la Wizara ni kuendelea kusimamia ukarabati na ujenzi wa miradi ya umeme nchini
*"Tutahakikisha Miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji umeme. Pia mtiririko wa maji umesaidia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza upungufu wa umeme baada ya Serikali kuchukua hatua madhubuti za kufanya matengenezo kwenye vituo vyetu vyote."* amesema Mbuttuka
Ameongeza kuwa hadi kufikia Januari 2024, Bwawa la Julius Nyerere linategemea kuzalisha Megawati za awali 235 na ifikapo Februari kuzalisha Megati 235 na kufikisha kiwango cha Megawati 470 na kuondoa upungufu wa upatikanaji umeme nchini.
"Serikali itaendelea kuweka mkazo na kuhakikisha tunaongeza kasi katika miradi ya usafirishaji na usambazaji wa umeme katika maeneo ya Tanga na hali itaimarika zaidi kwa kuunganisha njia ya Umeme kutoka Arusha hadi Tanga " amesema Mbuttuka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Balozi Meja Generali, Paul Kisesa Simuli,
amewahakikishia wawekezaji wa Mkoa wa Tanga hususan wazalishaji wa Saruji kuongeza kasi ya uwekezaji zaidi kwa kuwa Taifa halina tatizo la upungufu wa umeme kutokana na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini.
"Hapa kwenye huu Mradi wa New Pangani Falls tunazalisha Megawati 68 , hii inatokana na miundombinu iliyopo hapa. Bado tunaendelea kupunguza upungufu wa Megawati 470 na sasa hivi zimebakia Megawati 120 ili tuweze kufikia malengo, na tunaamini kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa ifikapo Aprili 2024 kukatika umeme itakuwa historia kwamba tulikuwa mgao wa umeme Tanzania" amesema Balozi Simuli.
Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dkt. David Mathayo. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, (aliyemwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.) Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
No comments:
Post a Comment