Mwonekano wa jengo jipya la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma ambalo ujenzi wake unaendelea jijini Dodoma |
Na. Rainer Budodi na Veronica Mwafisi-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewasisitiza wakandarasi wanaojenga majengo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.
Mhe. Simbachawene amesema hayo kwa nyakati tofauti leo tarehe 15 Novemba, 2023 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo jijini Dodoma.
Aidha, Mhe. Simbachawene amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi na kwa wakati kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi kwa taasisi zilizo chini ya ofisi yake.
“Majengo haya yameanza kujengwa wakati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani na kulikuwa na mtikisiko wa uchumi na majanga mbalimbali duniani lakini hakusitisha kuleta fedha za ujenzi wa majengo haya. Hivyo, hatuna budi kuendelea kumuombea dua na sala ili aendelee kutuongoza kwa hekima na busara” amesema Mhe. Simbachawene.
Pia, amewapongeza TAKUKURU kwa ubunifu wa kulipa Mkandarasi kwa mfumo wa milestone lengo likiwa ni kuimarisha mtiririko wa fedha kwa mkandarasi kulingana na kazi inavyofanyika na kutoa fursa ya kukamilisha jengo kwa wakati.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema kwa kibali cha mamlaka ya bajeti, Mshitiri ameridhia malipo ya mkandarasi yafanyike kwa kutumia utaratibu wa milestone badala ya kutumia utaratibu wa vyeti vya malipo ya mpito (interim payment certificates) ili kukamilisha mradi wa ujenzi ifikapo Julai, 2024.
Kamishna Hamduni ameongeza kuwa, mpango wa kutumia utaratibu wa malipo kwa milestone utaanza tarehe 4 Disemba, 2023 na utatoa fursa kwa mkandarasi kulipwa kiasi cha fedha kulingana na kazi alizopanga kuzifanya na kuzikamilisha kwa asilimia 100.
Katika hatua nyingine, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Simbachawene amesema katika kipindi cha miezi kumi (10) mkandarasi ambaye ni Kampuni ya CRJE (East Africa) amefanya kazi kubwa, kwa haraka na ufanisi ya ujenzi wa ofisi hiyo.
“Ninawasisitiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kusimamia kwa ukamilifu ujenzi huu ili jengo likamilike kama linavyoonekana kwenye mchoro wa jengo hili” amesema Mhe. Simbachawene.
Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama amesema ujenzi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la sakafu sita (6), nyumba ya mlinzi, chumba cha kuhifadhi mitambo ya umeme, kibanda cha kukusanya taka, ujenzi wa uzio na utengenezaji wa mandhari ya nje ya jengo ambapo hadi sasa mkandarasi amefikia asilimia 50 ya kazi zote.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma ulianza terehe 12 Januari, 2023 na Mkadarasi akiwa ni Kampuni ya CRJE (East Africa) na kwa mujibu wa mkataba anatakiwa kukabidhi jengo hilo ifikapo Septemba, 2024.
No comments:
Post a Comment