Na Carlos Claudio - Dodoma
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesisitiza upandaji wa miti katika vyanzo vya maji ili kuboresha mazingira yatakayopelekea upatikanaji wa maji ya uhakika.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo Novemba 27,2023 alipotembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa majisafi Nzuguni jijini Dodoma na kuridhishwa na utekelezaji wake.
Amesema Dodoma inaanza kupata matumaini na leo matokeo ya matumaini yanaanza kutoa matunda kwani amekuwa akisikitishwa na ukosefu wa maji katika Jiji la Dodoma ikiwa ni makao makuu ya nchi na viongozi wote wa kitaifa wanakaa hapa pamoja na wageni wanaokuja kupata huduma hapa hivyo ni vyema huduma ya maji ipatikane kwa uhakika.
“Niwapongeze sana DUWASA pia kwa kazi nzuri mmeifanya mradi huu mmeanza sio muda mrefu kama mlivoelezea miezi michache lakini sasa hivi tunashuhudia mradi unaenda kwenye hatua za umaliziaji”.
Na kuongeza kuwa “Leo tuna majawabu hatuna lugha za kisiasa tumefundishwa takwimu tuongee hasa leo tunaenda kuongea kwa takwimu subirini tarehe 1 Januari mtaanza kuona maji yanapatikana lakini kabla ya hapo mtaona kidogo kidogo kwa maana tunaendelea na majaribio lakini tukisema tarehe 1 Januari tuna uhakika sasa Ilazo hamna shida ya maji, Nzuguni hakuna shida ya maji, Mwangaza hakuna shida ya maji na wanaoendelea kujenga Maomanyika hakuna shida ya maji jambo ambalo kwenye mkoa wa Dodoma linakuwa historia,”amesema Mhe. Senyamule.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye Jiji la Dodoma kwenye miradi mkakati na ili itekelezwe inahitaji sana uwepo wa maji lakini pia maafisa waandamizi wa serikali pamoja na watumishi wa umma wanapohamia Dodoma wanataka uhakika wa maji kwaajili ya maisha yao.
“Ukichanganya na mahitaji mengine kwenye shughuli za mifugo, kilimo, makazi ya nyumbani, kwenye viwanda kwa hiyo hii miongoni mwa changamoto kubwa kabisa na kama kuna maeneo ambayo changamoto hii imewahi kuwa ni kubwa wananchi wanalalamika sana ni maeneo ya Nzuguni kwa hiyo nichukue nafasi hii kumshukuru yeye kuridhia kutoa fedha bilioni 4.8 kwaajili ya mradi huu kupitia Wizara pamoja na usimamizi unaofanywa na DUWASA.”amesema Mhe. Shekimweri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo ulikuwa ukamilike tarehe 30 Oktoba lakini mpaka hivi sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji na una lengo la kuongeza maji asilimia 11.7 katika uzalishaji ni takribani asilimia 50.
“Tayari tuko kwenye hatua za majaribio za kujaribu mradi huu na watu wameshaanza kupata maji wa Nzuguni A, Nzuguni B, Nzuguni C wameshaanza kupata huduma hii japo sio kwa muda wote mfululizo kwa sababu tupo kwenye majaribio tunaingiza maji tunapeleka kwa wananchi yanapoonekana kuna kitu cha kurekebisha mkandarasi anarekebisha”.
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph aliongezea na kusema wakati wanamalizia mradi huo wapo katika awamu ya pili ya uchimbaji wa visima vingine vikubwa vitano kwaajili ya kuongeza maji sio chini ya asilimia 15 mpaka 20 ili kupunguza uhaba wa maji na kubakiza asilimia kati ya 20 hadi 30 kwani wamefanya majaribio na kugundua umbali wa mita 120 mpaka 300 kuna maji mengi kama bahari na wameanza kuchimba kisima cha kwanza cha majaribio na mpaka itakapofikia Disemba wataweza kupata ukweli kama maji yapo na salama kwa matumizi ya binadamu.
No comments:
Post a Comment