Na.Samwel Mtuwa - Shinyaga.
Taarifa ya kamati ya wataalam iliyoundwa kufanya uchambuzi wa mikataba kati ya Vikundi vya wachimbaji wadogo wa madini na mwekezaji kwenye leseni za uchimbaji mdogo zilizopo katika eneo la Mwakitolyo mkoani Shinyanga imebaini sehemu kubwa ya maduara hayapo katika hali salama ya uchimbaji.
Hayo yamebainishwa leo oktoba 11,2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya uchunguzi kutoka Wizara ya Madini Mhandisi Ally Samaje wakati akiwasilisha taarifa ya uchunguzi kwa Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde mkoani Shinyanga.
Akizungumza kuhusu vibali vya usafirishaji malighafi Mhandisi Samaje amesema kuwa jumla ya vibali 1578 ambavyo vilisafirisha Tani 790,000 za mbale ambapo kati ya hizo tani 271,278, sawa na asilimia 34 zilitoka eneo la Nyaligongo.
Sambamba na hapo kamati imebaini kuwa uchimbaji wa pamoja (co-existence) kati ya Wachimbaji wadogo na Wawekezaji wabia inawezekana ambapo Wawekezaji watakuwa wanachimba kina cha mita 130 chini ya ardhi huku Wachimbaji wadogo wakichimba kuanzia juu hadi mita 60 chini ya ardhi, kina ambacho wanaweza kumudu na kitaweka tofauti ya takribani mita 70 kati yao na Wawekezaji umbali ambazo ni salama.
Akielezea juu usalama wa migodi Mhandisi Ally Samaje amesema kuwa kamati imebaini kuwa maeneo mengi ya maduara usalama ni mdogo hususani katika eneo la uchimbaji katika mlima Nyilagongo kutokana na maduara mengi kuporomoka na kuacha miamba hatarishi inayoning'nia.
Kutokana na hali hiyo, katika leseni 7 za uchimbaji mdogo zilizofanyiwa uchambuzi kuna maduara 65 tu ambayo ni hai kati ya maduara 1297. Hivyo, Kamati imeshauri miamba inayoning'nia ikatwe na kuondolewa ili kuweka mazingira salama ya kufanya kazi kwa usimamizi wa Mkaguzi Mkuu wa Migodi.
Aidha, taarifa imebainisha pia kutokana na kuendesha uchimbaji wa pamoja hakuna mchimbaji yeyote atakayeondolewa na kwamba usalama ukiimarishwa maduara mengi yatafanya kazi na hivyo kupata malighafi nyingi kwa ajili ya mitambo ya uchenjuaji iliyoko Mwakitolyo.
Mnamo Septemba 28, 2023 Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali aliunda timu ya wataalam ili kuchambua Mikataba kati ya Vikundi vya Wachimbaji wadogo na mwekezaji katika vitalu na leseni za uchimbaji dhahabu katika eneo la Mwakitolyo.
*VISION2030:MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI*
No comments:
Post a Comment