Sehemu ya Mafundi wa Kampuni ya China Railway Major Bridge Engineering Limited wakiwa kazini katika mradi wa maboresho ya bandari ya Kemondo, mkoani Kagera. |
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mara baada ya kukagua maendeoe ya mradi wa bandari ya Kemondo, mkoani Kagera. |
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa nguzo za gati katika bandari ya Bukoba. Ujenzi wa bandari hiyo unagharimu takribani shilingi bilioni 19 na unatarajiwa kukamilika mwezi mei mwakani. |
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi Kampuni ya China Railway Major Bridge Enginnering Limited (CRMBEG) kuhakikisha mradi wa maboresho katika Bandari ya Bukoba na Kemondo unakamilika mwezi mei mwakani ili kuruhusu meli ya MV. Mwanza kuweza kutoa huduma katika bandari hizo.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi hiyo mkoani Kagera Waziri Prof. Mbarawa amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha shughuli za uchukuzi baina ya bandari hiyo, mikoa ya kanda ya Ziwa na nchi Jirani zinazunguka mikoa hiyo.
“Nawapongeza kwa hatua iliyofikiwa lakini niwakumbushe kuwa Ujenzi wa meli ya MV. Mwanza uko katika hatua mbalimbali za kukamilishwa na itakapokamilika itatumia bandari hizi mbili kutoa huduma hivyo lazima tuongeze kasi ya ujenzi hususani kwenye gati angalau moja kwa kila bandari ili kuruhusu meli yetu ya MV Mwanza kutoa huduma itakapokamilika’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na mradi huo kuhakikisha vifaa maalum vya kuongozea meli vinawekwa katika Viktoria ili kuziwezesha kutoa huduma katika hali ya usalama.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanali Wilson Sakulo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza fedha katika usafiri majini na miundombinu yake kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutachochea ukuaji wa biashara kwa mikoa ya kanda ya Ziwa.
Aidha, Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Dar Al Handah Consultants Joshua Lesha amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa watahakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo miwili sababu sehemu kubwa ya vifaa vya ujenzi vipo kwenye eneo la mradi.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Juma Kijavara amesema miradi inayohusisha maboresho ya bandari ya Kemondo na Bukoba umefikia asilimia 25 na TPA itahakikisha inamsimamia mkandarasi ili akamilishe mradi huo kwa wakati.
Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Kemondo na Bukoba unaohusisha Ujenzi wa gati, majengo ya abiria na miundombinu mingine utagharimu takribani bilioni 40 na unatajiwa kukamilika mwakani.
No comments:
Post a Comment