Na Elimu ya Afya kwa Umma.
Wito umetolewa kwa Serikali pamoja na wadau wa sekta ya Afya kuibeba na kuifanya ajenda ya elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza iwe ya kudumu lengo ni kupambana na hatari ya magonjwa yasiyoambukiza katika Jamii.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Bi. Ziada Sellah ambaye ni Muuguzi Mkuu wa Serikali alipokuwa akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu katika Ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Ushauri wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Elimu ya Afya na Lishe Shuleni.
"Kama alivyosema Kaimu Mkurugenzi wa Kinga kwasasa Magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yanawapata hata watoto wadogo zamani ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu walikuwa wanapata matajiri lakini kwasasa wanapata hata watoto wadogo kwa hiyo ni vyema kuwa na ajenda ya kudumu na hii unaweza kuifanya hata unapokuwa kwenye sherehe mbalimbali kwasababu pale kuna Pilau nyama Kuna kuku na Kuna vitu vingi ni muhimu kutoa Elimu katika eneo hilo kuhusu ulaji" amesema Bi Sellah
Aidha Bi. sella ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha. Afua za Kinga dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza, na mgonjwa ya kuambukiza kwa kutoa Hamasa na Elimu ya Jinsi ya kujikinga. Pia katika kukabiliana na Malaria Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea na zoezi la ugawaji wa vyandarua Nchi nzima lakini pia Elimu na Hamasa kuhusu Chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi imeendelea kutolewa na kwa lengo la kuwakinga mabinti dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi ambapo hadi Sasa asilimia 87 ya mabinti wenye umri wa miaka 14 wamepatiwa chanjo dozi ya kwanza na asilimia 67 wamepata chanjo dozi ya pili .
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Dkt. Tumaini Haonga amesema kuwa Wizara ya Afya imeimarisha Mpango wa Taifa wa Huduma za Elimu ya Afya na Lishe ili kuweza kuwafikia wanafunzi wengi kuanzia Shule za Msingi, vyuo vya kati na vyuo Vikuu.
"Kwasasa kumekuwa na changamoto ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto wadogo hasa kisukari aina ya pili kwa hiyo kupitia mpango huu tutaweza kuwafikia wanafunzi wengi na kuwapatia elimu kuhusu Afya lakini pia malezi yao" amesema Dkt. Haonga
Kikao kazi hiki cha Kamati ya Ushauri wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Elimu na Lishe Shuleni kimeshirikisha Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ,Ofisi ya Rais Tamisemi ,Wadau wa maendeleo na wawakilishi kutoka Taasisi za Elimu ya Juu pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali.
No comments:
Post a Comment