MKOMI AWATAKA WAAJIRI KUSHIRIKI WENYEWE KIKAO KAZI CHA RASILIMALIWATU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 26, 2026

MKOMI AWATAKA WAAJIRI KUSHIRIKI WENYEWE KIKAO KAZI CHA RASILIMALIWATU


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi amewataka Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu serikalini kushiriki wenyewe kikao kazi cha kitaifa kitakachofanyika jijini Dodoma Juni 1 hadi 3, 2026 ili kupata maelekezo mahsusi ya usimamizi wa rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Bw. Mkomi amesema kikao hicho kitawakutanisha Wakurugenzi na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kujadili namna bora ya kuongeza ufanisi, uwajibikaji na usimamizi wa watumishi wa umma.

Amesema kikao hicho kitafanyika katika Ukumbi wa Mabele Hall chini ya kaulimbiu isemayo “Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Ulio Sikivu, Jumuishi, wenye Matokeo na Uwajibikaji Kuelekea Dira 2050.”

Kwa mujibu wa Bw. Mkomi, kikao hicho cha kila mwaka pia kitajadili matumizi ya mifumo ya kidijiti ikiwemo e-Uhamisho, e-Watumishi, e-Utendaji, e-Mrejesho pamoja na HR Assessment ili kuimarisha utendaji kazi serikalini sambamba na kuendana na vipaumbele vya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.

Aidha, amesema viongozi watakaoshiriki watapatiwa maelekezo mbalimbali yanayohusu usimamizi wa rasilimaliwatu, huku akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya uwakilishi kutokana na umuhimu wa kikao hicho.

Bw. Mkomi amesema mgeni rasmi katika kikao hicho anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete.


No comments:

Post a Comment