OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi wote wa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha miradi ya Afya na Elimu iliyopata fedha inakamilika ifikapo Disemba 31,2023.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo kwenye hafla ya uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 - 2025 katika Jimbo la Vunjo kwa kipindi cha mwaka 2022/23 iliyofanyika mkoani humo.
Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan ni ya Elimu na Afya yeye ameshatekeleza jukumu lake sasa kazi ni kwa viongozi kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kabla ya Disemba 31,2023.
"Kiongozi ambaye hatakamilisha mradi hiyo mpaka kipindi hicho atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye nafasi hiyo ili tuwape wengine wenye uwezo wa kufanya kazi."
"Nafasi hizi tumepewa kwa kuaminiwa sana na inabidi tufanye kazi kwa kujutoa ili kuwahudilia wananchi sasa wewe unapewa fedha za miradi unakaa nazo na miradi haijakamilika huku wananchi wanashindwa kupata huduma kwa sababu mtu mmoja tu ameshindwa kutekeleza majukumu yake huyu hatuwezi kumfumbia macho lazima achukuliwe hatua," amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Ameongeza kuwa "Kila mmoja ajitafakari je anatekeleza majukumu yake ipasavyo na ukiona huwezi kwenda na kasi yetu ni bora ukae pembeni kwa kuwa malengo yetu ni kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma bora kupitia utendaji kazi wetu."
Mhe. Mchengerwa yupo ziara ya kikazi kwenye Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Singida, Kagera, Geita na Mwanza
No comments:
Post a Comment