
Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Joseph Sambali (mwenye fulana nyeusi) akielezea ufanisi wa majiko banifu yanayosambazwa kwa bei ya ruzuku kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko (wa pili kulia) wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa majiko hayo mkoani humo Desemba 18, 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko akipokea jiko banifu kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Tango Energy Limited iliyoshinda zabuni ya kusambaza majiko hayo kwa bei ya ruzuku mkoani humo, Musa Msofe wakati wa uzinduzi wa mradi Desemba 18, 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko ametoa wito kwa wananchi wa Katavi kuchangamkia fursa ya kununua majiko banifu kwa bei ruzuku ya shilingi 7,500 yanayosambazwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kulinda afya, kuokoa misitu na kuhifadhi mazingira.
Ametoa rai hiyo Desemba 18, 2025 Mkoani Katavi wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza majiko banifu ya ruzuku yapatayo 3,126 mkoani humo unaotekelezwa na Kampuni ya Tango Energy Ltd ya Jijini Dar es Salaam unaoratibiwa na kusimamiwa na REA wenye thamani ya shilingi milioni 156.3 ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034).

“Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi, majiko haya ni kwa ajili yenu na yameuzwa kwa bei ya ruzuku kwa maana ya kwamba Serikali imelipia zaidi ya shilingi 50,000 lakini mwananchi analipia shilingi 7,500 pekee, naomba mchangamkie fursa hii,” amesisitiza Mhe, Mrindoko.
Mhe. Mrindoko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amejielekeza katika kuhakikisha kwamba wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia.
Alisisitiza wananchi wa Katavi kuhakikisha maono na maelekezo ya Rais ya kuendelea kutunza misitu yanatekelezwa na kwamba kupitia mradi wa kusambaza majiko banifu kwa bei ya ruzuku utawezesha uhifadhi wa misitu.
“Tunamshukuru Rais na tunamhakikishia kwamba afua zote zinazohusiana na utunzaji wa mazingira, utunzaji wa misitu kwa kusaidiana na Wakuu wa Wilaya na watendaji tutahakikisha jambo hili linafanikiwa kikamilifu ili ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia kama inavyoelekezwa,” alisema Mhe. Mrindoko.
Akitambulisha mradi, Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali alisema majiko hayo yatauzwa kwa shilingi 7,500 badala ya shilingi 59,000 kwakuwa Serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya 85% sambamba na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika majiko hayo ili kumpa unafuu mwananchi.
“Kabla ya ruzuku jiko moja lilikuwa likiuzwa kwa shilingi 59,000 na baada ya Serikali kuweka ruzuku likauzwa kwa shilingi 8,850 lakini sasa baada pia ya kuondoa kodi ya VAT jiko moja hapa Katavi litauzwa kwa shilingi 7,500 pekee," alibainisha Dkt. Sambali.
Alisema katika kila Wilaya majiko banifu 1,042 yatasambazwa ambayo jumla yake ni majiko 3,126 ambapo alizitaja wilaya hizo kuwa ni Mpanda, Mlele na Tanganyika.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Tango Energy Ltd, Musa Msofe alisema wamejipanga ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwamba majiko hayo yatauzwa kwa bei ya ruzuku kwa mwananchi mwenye kitambulisho cha Taifa (NIDA) na kwamba majiko hayo yana udhamini (warranty) wa mwaka mmoja.



No comments:
Post a Comment