“TAFITI ZIELEKEZWE KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA UHIFADHI WA WANYAMAPORI NA MAENDELEO YA UTALII” MHE. KAIRUKI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, December 6, 2023

“TAFITI ZIELEKEZWE KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA UHIFADHI WA WANYAMAPORI NA MAENDELEO YA UTALII” MHE. KAIRUKI.


Na Happiness Shayo- Arusha

Serikali imeitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kuelekeza nguvu zake katika kufanya tafiti zitakazotatua changamoto za uhifadhi wa Wanyamapori na Maendeleo ya Sekta ya Utalii nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Kongamano la 14 la Kimataifa la Kisayansi linalofanyika leo katika ukumbi wa AICC jijini Arusha .


“Tafiti zinapaswa kuelekezwa katika kushughulikia changamoto za migogoro ya binadamu na wanyamapori, upotevu wa makazi ya wanyamapori, kuziba kwa shoroba za wanyamapori, mimea vamizi, magonjwa ya wanyamapori, na kupungua kwa idadi ya wanyamapori katika baadhi ya Maeneo Tengefu. ” Mhe. Kairuki amesema.

Ameongeza kuwa sehemu nyingi zinazoongoza kwa utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni matokeo ya taarifa za utafiti wa muda mrefu. 


Kufuatia hatua hiyo Mhe.Kairuki ameitaka TAWIRI kufanya tafiti za kimkakati katika ukanda wa Kusini ili nako kuweze kukua kiutalii kama ilivyo Kaskazini.

Amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha inatangaza utalii, kama inavyothibitishwa kupitia Filamu ya ' TANZANIA: The Royal Tour'. 

Amesema kutokana na filamu hiyo, idadi ya watalii imeendelea kuongezeka kutoka 1,711,625 (Watalii wa Ndani- 788,933 na Watalii wa Kimataifa- 922,692) mwaka 2021 hadi 3,818,180 (Watalii wa Ndani-2,363,260 na Watalii wa Kimataifa - 2020,2024) na Watalii wa Kimataifa 2025. % na inatarajiwa kufikia Watalii Milioni 5 mnamo 2025 kulingana na Ilani ya Chama Tawala.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amesema Serikali imedhamiria kuiongeza fedha TAWIRI ili kutekeleza miradi ya kimkakati ya utafiti kwa ajili ya uhifadhi na utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi 

“Ili kufanikisha hilo, nakubali pendekezo la kuanzishwa kwa mfuko wa utafiti wa TAWIRI kupitia michango, ushirikishwaji wa wadau na ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP)” Mhe. Kairuki amesisitiza

Kongamano hilo la mwaka huu lenye kauli mbiu “ Maisha jumuishi baina ya binadamu na wanyamapori kwa uhifadhi wa bioanuwai na kwa maendeleo kiuchumi na ustawi wa jamii”limehudhuriwa na Watafiti, waadau wa uhifadhi na utalii, wanasayansi ,vyuo na vyuo vikuu kutoka nchi 22.


No comments:

Post a Comment