Na Mwandhi wetu Msomera Tanga.
Wananchi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro waliohamia Kijiji cha Msomera mkoani Tanga wameanza kunufaika na ardhi waliyopewa na Serikali kwa kulima mazao mchanganyiko kwa ajili ya chakula na biashara.
Katika Msimu huu wa kilimo wananchi hao wamelima mazao mbalimbali ambayo ni Mahindi, maharage, Mbaazi, choroko, mihogo, mbogamboga, matunda na migomba ambayo yote imeonekana kustawi katika ardhi ya Msomera.
Mzee Saitoti Lekera mwananchi aliyehamia kutoka Kijiji cha Kapenjiro Ngorongoro kwenda Msomera anaeleza kuwa katika eneo alilopewa na Serikali ekari 2.5 zilizoko kwenye Nyumba anayoishi pamoja na ekari 5 alizopewa kwa ajili ya shughuli za kilimo, katika msimu uliopita pamoja na mvua kuwa chache alilima na kupata gunia 20 za mahindi ambayo hadi sasa anayatumia kwa Chakula na kuuza kidogo kwa ajili ya mahitaji ya Nyumbani.
“Msimu uliopita pamoja na ugeni wangu katika eneo hili na mvua kuwa chache nilipata gunia za mahindi 20, hadi sasa bado nina gunia 8 za akiba nyumbani kwangu, na msimu huu wa vuli nimelima tena na mvua zimekuwa nyingi hivyo natarajia kuvuna mazao mengi zaidi katika miezi miwili ijayo.
Kwa msungi huo utaona ni jinsi gani mimi na familia yangu tutasahau habari ya njaa hata hata nisipolima kwa miaka miwili ijayo” amebainisha mzee Lekera.
Katika Shamba lake Mzee Lekera tofauti na maahindi amepanda pia maharage, Choroko, mbaazi pamoja na kuanzisha ufugaji wa kuku wa kienyeji ambao wanapata chakula cha kutosha katika eneo lake.
Kwa upande wake Bw. Ngorisa Melubo aliyehama kutoka Kijiji cha Olbalbali Ngorongoro anabainisha kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na ardhi kuwa na rutuba ya kutosha ameshalima jumla ya ekari 4 za mahindi, mihogo na kupanda ekari 3 za majani kwa ajili ya Mifugo.
“Changamoto ya Ngorongoro kulikuwa na kugombania malisho kwa wanyamapori na mifugo, hapa hali ni tofauti maana ardhi ni nzuri mvua zimenyesha na majani ya malisho yapo kila mahala nikienda kuchunga ndani ya saa 6 mbuzi na ng’ombe wangu wanakuwa wameshiba narudi kupumzika” ameongeza Melubo.
Mama Christina Huho katika Shamba lake ameamua kupanda mazao mchanganyiko ikiwemo mahindi, migomba, matunda aina mbalimbali, mihogo, maharage, nyanya pamoja na Mbogamboga ambazo zimekuwa msaada katika Maisha yao.
Wananchi hao wameendelea kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumuita mkombozi wao kwa kuwatoa jangwani na kuwahamishia kwenye ardhi ya kanani, ardhi yenye rutuba inayokubali kila zao
“ Rais huyu anapenda watu wake, uamuzi wa Serikali kutuleta hapa umetuondolea utapiamlo na njaa, ambao kwa sasa tuna chakula cha kutosha kitu ambacho kimefanya afya zetu na watoto kuimarika na tuko huru tofauti na tulivyokuwa kwenye eneo la Hifadhi" ameeleza mmoja wa wananchi hao.
No comments:
Post a Comment