
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dkt Rhimo Nyansaho (Mb), Tarehe 02 Januari, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Mheshimiwa Bishwadip Dey katika ofisi ndogo za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga, jijini Dar-es-salaam.
Mheshimiwa Bishwadip Dey alitumia mkutano huo kujitambulisha na kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huo na kuahidi kushirikiana naye katika kudumisha mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na India hususani katika eneo la Diplomasia ya ulinzi na usalama.
Balozi Bishwadip Dey ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kudumisha mahusiano haya na kuahidi kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha mahusiano haya yanazidi kuchanua kwa faida ya nchi hizo mbili na watu wake.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, amemshukuru Balozi Dey kwa kufika Wizara ya Ulinzi na JKT na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na India, na akamhakikishia Balozi Dey, kuwa Wizara ya Ulinzi na JKT itaendelea kutekeleza kwa vitendo makubaliano yote ambayo nchi hizo zimekubaliana katika sekta ya ulinzi.
Wizara za Ulinzi za Tanzania na India kupitia Majeshi ya nchi mbili hizo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo mafunzo, mazoezi ya pamoja, kutembeleana na kubadilishana uzoefu, miradi ya kimkakati pamoja na kubadilishana wakufunzi katika vyuo vya kijeshi. Uhusiano kati ya Tanzania na India uliasisiwa baada ya uhuru wa Tanganyika ambapo India ilifungua Ubalozi wake jijini Dar es Salaam mwaka 1961 na mwaka uliofuatia, 1962, Tanzania nayo ilifungua ubalozi wake nchini India.


No comments:
Post a Comment