
Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Bodi ya Nyama Tanzania imeandaa mpango maalum wa kuhamasisha wachomaji nyama katika minada mbalimbali nchini kutumia nishati safi ya kupikia kwa lengo la kupunguza matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira pamoja na kulinda afya za wachomaji nyama na jamii kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kumtembelea mdau wa Nishati safi ya kupikia, Matima Investment Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, amesema mdau huyo anajihusisha na utengenezaji wa majiko maalum ya kuchomea nyama yanayotumia gesi, ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya.
Katika ziara hiyo, Bw. Mlay alikutana na wataalamu kutoka Bodi ya Nyama Tanzania pamoja na Meneja wa Benki ya CRDB, ambapo walijadili mikakati mbalimbali ya kuhakikisha minada yote ya kuchomea nyama nchini inahamia katika matumizi ya majiko ya kisasa yanayotumia nishati safi.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia hayalindi mazingira pekee, bali pia yanaboresha afya na kuongeza ufanisi katika shughuli za wachomaji nyama. Kupitia ushirikiano na Bodi ya Nyama Tanzania, tutaendelea kuwahamasisha wachomaji nyama katika minada mbalimbali kutumia nishati safi, kwani bodi hiyo ina jukumu la kusimamia na kuwaendeleza wadau wa sekta ya nyama,” amesema Bw. Mlay.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo hususani taasisi za kifedha na benki, kuwawezesha wachomaji nyama kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili waweze kumudu gharama za ununuzi wa majiko ya kisasa. Hatua hiyo itawawezesha wajasiriamali hao kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia teknolojia safi na rafiki kwa mazingira.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Mkoa wa Pwani, Bi. Rose Kazimoto, amesema benki hiyo iko tayari kushirikiana na wachomaji nyama pamoja na watengenezaji wa majiko ya nishati safi kwa lengo la kuongeza uzalishaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema CRDB itaangalia namna bora ya kuwawezesha wachomaji nyama kupata mikopo, jambo litakalosaidia kulinda mazingira na kuboresha afya zao.
Hata hivyo, amewasisitiza wachomaji nyama kujisajili katika Bodi ya Nyama Tanzania na kufanya kazi katika mfumo uliopangwa (organized) ili kurahisisha ufuatiliaji na upatikanaji wa mikopo.
Bi. Kazimoto ameongeza kuwa kutokana na hali ya wachomaji nyama wengi kuhamahama, ni vyema wakaunda vikundi vinavyodumu kwa angalau miaka mitatu. Amesema Mnada wa Loliondo tayari umejipanga vizuri na una sifa za kupata mikopo kutoka CRDB Bank.
Naye Afisa Dawati wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Bodi ya Nyama Tanzania, Bi. Pendo Msaki, amesema bodi hiyo imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika minada ya nyama nchini.
Ameeleza kuwa Bodi ya Nyama Tanzania iko katika hatua za mwisho za kuandaa waraka wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa katika minada ya nyama, hatua inayolenga kulinda mazingira na kuboresha afya za wachomaji nyama.
Aidha, amewasisitiza wachomaji nyama wote kujisajili katika Bodi ya Nyama Tanzania ili wapate ithibati na kutambulika rasmi.
Ameongeza kuwa bodi hiyo itaanza kusambaza majiko ya nishati safi kwa mkopo katika minada ya Loliondo–Kibaha pamoja na Pugu jijini Dar es Salaam, kama sehemu ya utekelezaji wa mpango huo.

No comments:
Post a Comment