SERIKALI YATENGA SH. BILIONI 125 ZA MABWAWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 2, 2026

SERIKALI YATENGA SH. BILIONI 125 ZA MABWAWA



SERIKALI imetenga sh. bilioni 125 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa saba katika mikoa ya Morogoro na Dodoma pindi kazi ya upembuzi yakinifu itakapokamilika.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo wakati alipopewa nafasi na Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba awasalimie wakazi wa Gulwe, wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma mara tu baada ya kukagua athari za mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Akielezea mikakati ya Serikali, Waziri Chongolo amesema kazi inayofanyika kwa sasa ni kutafuta namna ya kuhifadhi maji ili yaweze kutumika kwa shughuli za kilimo katika wilaya za Mpwapwa na Kilosa.

“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa bwawa la Msagali umekamilika, kazi inayofuata ni ujenzi wa mifereji na miundombinu ya umwagiliaji. Awamu ya pili itakuwa na kazi ya upanuzi wa bwawa ili tuweze kuhifadhi maji mengi zaidi,” amesema.

“Serikali imetoa shilingi bilioni 125. Ndani ya miezi mitatu hadi minne, tukikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, tunaanza kazi ya ujenzi wa mabwawa ya Kidete, Kimagai, Buigiri, Ikoa, Hombolo, Dabalo na kukamilisha hili la Msagali. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji katika bonde linalounganisha Mpwapwa, Kilosa na Mvomero,” amefafanua.

Naye, Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Omari alipopewa nafasi kuzungumza na wananchi hao, alisema Serikali imeshatoa sh. bilioni 5.3 ambazo gharama za awali za ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mpwapwa hadi barabara kuu ya Dodoma - Morogoro. Amesema gharama zote za ujenzi wa barabara hiyo ni sh. bilioni 53.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa reli ya kisasa ipo salama na Shirika la Reli litaendelea kuchukua tahadhari zote kwa ajili ya usalama wa abiria wanaotumia huduma hiyo.

“Reli yetu iko salama. Kwa sasa tunafanya tathmini ya kina kutoka Morogoro hadi Dodoma ili kujiridhisha na usalama wa njia ya treni. Watakamilisha kesho na kuanzia kesho usiku, safari zitaanza,” amesema.

Akihitimisha maelezo ya mawaziri walioambatana naye kwenye ziara hiyo ya siku moja, Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba amesema jambo linalofanywa na Shirika la Reli nchini (TRC) kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi ni la msingi ili kujiridhisha na usalama wa reli hiyo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wakati akikagua athari za mvua katika maeneo ya Tindiga, Kidete, Godegode mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma leo (Ijumaa, Januari 02, 2026), Dkt Mwigulu amesema ujenzi wa mabwawa hayo utakuwa ni suluhisho la kudumu la mafuriko katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro.

Amesema kuwa uamuzi wa Serikali wa kujenga mabwawa hayo katika eneo la Kidete ni uthibitisho wa kuwa Serikali ipo makini katika kuhakikisha inakabiliana na changamoto za wananchi na imeshachukua hatua kupata suluhisho la kudumu.

No comments:

Post a Comment