Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Ujenzi Mhe.
Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),
Dkt. Jim Yonazi pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamefika katika
kijiji cha Gendabi kata ya Gendabi Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara eneo
yalipotokea maporomoko ya tope Leo tarehe 04 Disemba 2023.
Viongozi hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa Manyara Mhe. Queen
Sendiga kufika katika Kijiji cha Gendabi ambalo ni eneo liliothirika Maporomoko
ya tope kutoka Mlima wa Hanang yaliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 03 Disemba
2023.
Akiwa eneo la tukio hilo, Waziri Mhagama, amewaomba wananchi
hao kupokea pole ambazo zinatoka kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambaye aliagiza lazima KUfika eneo la tukio na
kuona nini kifanyike kwa dharura kuhusu uokoaji pamoja na makazi kwa waathirika
hao.
“Mambo haya yakitokea kuna mambo ya haraka yanatakiwa
yafanyike kwa dharura hivyo tumekuja na kushauriana namna ya kujipanga kwa
pamoja ili kufanikisha jambo hilo kwa uharaka”. Ameongeza Mhagama
Ameongeza kuwa, maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwanza kuona
namna gani wanaweza kuendelea kuokoa watu na kazi hiyo wanaendelea nayo vikosi
vya uokoaji, pia kuangalia namna gani ya kuweza kuwasitiri wenzetu
waliotangulia mbele ya haki.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeshaleta
wataalamu wa Miamba watatoa taarifa ya nini kilichotokea na nini kifanyike
katika mlima wa Hanang.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema
kazi ya kufungua miundombinu ya barabara inaendelea ili kurahisia kazi za
uokoaji na kufikisha huduma muhimu za kijamii katika meneo yaliyoathirika.
Amesema Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) tayari
wamefungua Barabara ya Singida-Babati ambayo awali ilikuwa haipitiki kutokana
na kujaa tope na magogo ya miti kutoka milimani.
No comments:
Post a Comment