Na Mwandishi Wetu
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Bw. Athuman Mbuttuka amesema ni jukumu la Serikali na Sekta Binafsi katika kuhamasisha upatikanaji wa Nishati Safi ya kupikia katika Taasisi za Serikali zinazolisha watu zaidi ya 100.
Naibu Katibu Mkuu, amesema hayo alipokuwa akiongoza kikao Cha Kamati Tendaji ya Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia unaofadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU) kilichofanyika Tarehe 14 Desemba, 2023 Jijini Dae es Salaam.
“Kamati yetu ina wajibu wa kufuatilia na kusimamia Utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ifikapo Januari, 2024 kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100”. Aliongeza Bw Mbuttuka akirejea maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa tarehe 1 Novemba 2022 wakati akizindua Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
Kikao hicho kilijadili mpango Kazi wa Mwaka 2024 na Miradi ya Uhamasishaji wa Matumizi Endelevu ya Nishati Safi ya Kupikia na Utunzaji wa Mazingira na Kupunguza Uharibifu. Miradi hiyo inatekelezwa na Serikali kupitia Sekta Binafsi.
Aidha, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga alitoa taarifa ya uzinduzi wa Program ya Uhamasishaji wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa ajili ya kuwasaidia Wanawake wa Africa (AWCCSP) uliofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira (COP28) uliofanyika Dubai na kuhudhuriwa na Wakuu wa nchi mbalimbali pamoja na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Kitengo cha Mazingira wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Wasimamizi wa Mradi huo wa Mfuko wa Maendeleo ya Mtaji wa Umoja wa Mataifa , Wajumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Taasisi ya Misitu ya Tanzania (TFS)
No comments:
Post a Comment