Kwa muda mrefu, benki za biashara na taasisi nyingine za fedha pamoja na kampuni za simu zilikuwa zinatoa msimbomilia unaojitegemea lakini serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanya jitihada kuiunganisha misimbomilia yote ili kumpa mteja unafuu.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Lipa Namba hiyo, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo (BoT), Lucy Charles Shaidi aliyepaswa kuwa mgeni rasmi, Meneja Mradi wa BoT, Mutashobya Mushumbusi amesema kasi ya mabadiliko yatokanayo na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwenye huduma za fedha inazidi kuongezeka duniani hivyo serikali inachukua hatua muhimu kuhakikisha Tanzania haiachwi nyuma kwa kuwawezesha wananchi wake kuendana na hali iliyopo.
“Kati ya vingi vinavyofanywa na serikali yetu kupitia Benki Kuu ya Tanzania ni kuweka sera na miundombinu madhubuti ili kuchochea ujumuishi wa kifedha nchini.
Huduma jumuishi za fedha huchangia katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja, biashara na uchumi wa Taifa kwa ujumla. Katika mazingira yanayoendelea kubadilika ya huduma za kifedha, maendeleo ya teknolojia yamepelekea Benki Kuu kutathmini na kubuni upya mbinu za usimamizi ili kuongeza ufanisi, uwazi na kukuza mazingira yanayohimiza uvumbuzi wa bidhaa na huduma,” amesema Mushumbusi.
Mwaka 2014 serikali ilifanya mabadiliko makubwa yaliyoiweka kwenye historia baada ya kuruhusu mteja wa mtandao mmoja wa simu kumtumia fedha mteja wa mtandao mwingine (interoperability) hali iliyorahisisha utumaji miamala kupitia simu za mkononi.
Mpaka mwaka huo, mteja wa kampuni moja ya simu alikuwa hawezi kumtumia fedha mteja wa mtandao mwingine lakini sasa inawezekana.
“Kwa muongo mmoja sasa, tumejijengea uwezo na kupata uzoefu wa kutosha katika eneo hilo.
Tarehe 12 Agosti 2022 Benki Kuu ya Tanzania ilitoa mwongozo kwa watoa huduma za fedha wote nchini kuhusu kuanzishwa na kutumika kwa Msimbomilia wa Taifa Tanzania 2022 (Circular on the establishment of Tanzania Quick Response CodeStandard - TANQR Code Standard 2022). Mwingiliano huu tunaamini utasaidia kuongeza kasi ya ulipaji wa kidijitali hivyo kupunguza matumizi ya fedha taslimu.
Nawapongeza Benki ya CRDB kwa kuwa wa kwanza kutekeleza maelekezo ya Benki Kuu ya Tanzania,” amesema Mushumbusi.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema siku zote ubunifu ndio nguzo kuu ya huduma za taasisi hiyo kubwa zaidi ya fedha nchini.
“Tunajivunia ubunifu ambao Benki yetu imefanya katika eneo hili.
Tulikuwa wa kwanza nchini kubuni na kuingiza sokoni huduma za TemboCard, SimBanking, SimAccount, internet banking, CRDB Wakala na malipo kupitia msimbomilia yaani QR Code. Hivi sasa zaidi ya asilimia 90 ya miamala ya wateja wetu inafanyika kupitia mifumo hii ya kidijitali,” amesema Raballa.
Hata katika uzinduzi huu wa msimbolia wa pamoja, Raballa amesema ni fahari kwa Benki ya CRDB kuonyesha njia kwa watoa huduma wengine wa fedha kutekeleza mwongozo uliotolewa na Benki Kuu ya Tanzania juu ya matumizi ya Msimbomilia wa Taifa (TANQR) kwani tayari baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia LIPA NAMBA na msimbomilia wamehamia kwenye mfumo huo lakini bado wanaweza kuwahudumia wateja wao tu kwa kuwa kampuni nyingine bado hazijahamia huko.
Benki ya CRDB inao wafanyabiashara zaidi ya 30,000 wanaopokea malipo kwa mfumo wa LIPA NAMBA na msimbomilia.
Kwa maboresho yaliyofanywa, ukiacha wateja wa kampuni nyingine wanaotaka kulipa kupitia LIPA NAMBA na msimbomilia, hata wage na watalii wanaotumia huduma za kampuni za kimataifa wataweza kulipa kwa urahisi hali itakayoongeza miamala kwa wafanyabiashara watakaokuwa na mfumo huo rafiki wa malipo.
No comments:
Post a Comment