WATUMISHI WA UMMA 440 KUNUFAIKA CHUO CHA TEHAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, January 29, 2024

WATUMISHI WA UMMA 440 KUNUFAIKA CHUO CHA TEHAMA


Na Carlos Claudio -Dodoma

Serikali imetoa nafasi kwa watumishi wa umma 440 ambao wanahitaji kujiendeleza kwenye sekta ya TEHAMA kuomba ufadhili wa masomo ya muda mrefu na muda mfupi ili kupata ujuzi zaidi kwenye sekta hiyo.

Pia imewatangazia vijana wote nchini wanaojua kusoma na kuandika kuomba nafasi za kujiunga na chuo cha TEHAMA kitakachojengwa Jijini Dodoma ili waweze kupata ujuzi kwenye masuala ya teknolojia na habari.

Akizungumza leo Jumatatu, Januari 29, 2024 na waandishi wa habari jijini Dodoma,Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Khamis Abdullah amesema chuo hicho kitakapokamilika kitadahili jumla ya wanafunzi 15,000 kwa mwaka hivyo ametoa wito kwa wananchi wote kutumia fursa hiyo kujipatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.


"Chuo hicho kitasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kwani sio vijana wote wamefanikiwa kusoma darasani na kufikia kiwango cha juu, kuna vijana wenye vipaji ambao hawajasoma hivyo kupitia chuo hiki vijana wengi watapatiwa ujuzi na kuweza kuendana na mapinduzi ya viwanda,” amesema Abdullah.


Amesema pamoja na ujenzi wa chuo hicho cha Nala lakini pia serikali inajenga chuo kingine cha Tehama kilichopo Buhigwe Mkoani Kigoma ambacho kitagharimu Sh80,000 bilioni.

Amesema lengo ni kuongeza ujuzi wa kitaaluma katika eneo la Tehama hususani mafunzo ya ujuzi na ubunifu katika eneo la Teknolojia zinazoibukia na kwamba ujenzi wa vyuo hivyo utachochea maendeleo katika mapinduzi ya viwanda ambayo ndio chachu ya ukuaji wa uchumi wa kidigitali duniani.

“Vyuo hivi vya Tehama vitakua kitovu cha taaluma, ujuzi, ubunifu, tafiti, maarifa na kukuza ujasiriamali wa kidijitali kitaifa na kimataifa ambapo vitaifanya Tanzania kuwa mahali pazuri pa kuvutia utalii wa kidijitali, kujifunzia, na kuongeza uwekezaji kutokana na upatikanaji endelevu wa jamii yenye maarifa yanayoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.”

Amesema kutokana na uhitaji huo Serikali imeamua kujenga chuo hicho ili kisaidie kutoa ujuzi kwa vijana wote wanaojishughulisha na Tehama ambacho kitatoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana na wabunifu nchini kama vile Teknolojia zinazoibukia, usalama wa mifumo ya mawasiliano pamoja na utengenezaji wa mifumo yake.

Serikali imeweka mpango wa ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watumishi wa Umma 500 kwenye kozi za kuongeza ujuzi kwenye masuala yanayohusu Tehama hususani eeknolojia zinazoibukia.

Amesema katika awamu ya kwanza jumla ya watumishi wa umma ishirini (20) wameweza kufadhiliwa katika mafunzo ya muda mrefu katika vyuo vikuu nje ya nchi ambapo kozi walizoenda kuongeza ujuzi ni kwenye masuala yanayohusu Tehama hususani teknolojia zinazoibukia.

Aidha Maprofesa kutoka vyuo vikuu vya Da es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Chuo Kikuu cha Sayansi na teknolojia (Must) watajengewa uwezo ili waweze kuendelea kutoa mafunzo katika vyuo walivyotoka wakati Chuo Mahiri cha Tehama kinaendelea kujengwa.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Ally Gugu amesema mkoa huo utatoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi wa chuo hicho ili malengo ya serikali yaweze kutimia.

Kwa upande wake makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka amesema chuo hicho kina ndaki inayoshughulika na mambo ya Tehama hivyo kitatayarisha wataalamu watakaoshiriki kuwafundisha vijana wanaokuja.

Amesema chuo hicho kimeshatenga jengo la kuanzia kutoa mafunzo ya Tehama wakati makao makuu yake bado yanajengwa kwa kuwa Udom ni sehemu ya rasilimali za serikali ambayo imewekenzwa kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment