DKT. BITEKO AMWAKILISHA RAIS SAMIA UWEKAJI WAKFU ASKOFU MPYA JIMBO KATOLIKI BUKOBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, January 27, 2024

DKT. BITEKO AMWAKILISHA RAIS SAMIA UWEKAJI WAKFU ASKOFU MPYA JIMBO KATOLIKI BUKOBA


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, leo amemwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Mhashamu
Jovitus Mwijage ikiwa ni tukio la kihistoria kutokana na kupita
takriban miaka 50 kutoka kufanyika sherehe kama hiyo ya uwekaji wa
wakfu.

 Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa na Mbunge wa Bukoba Mjini ambaye
pia ni Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato.


Akitoa Salam za Dkt. Samia kwa waumini na wananchi waliohudhuria sherehe hizo, Dkt. Biteko ameeleza kuwa, Rais ataendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ili kwa pamoja walete maendeleo nchini.

Amesema, Rais anatambua kuwa bado kuna changamoto mbalimbali nchini ambazo Serikali inafanya kila jitihada ili kuzindoa lakini hili litafanyika kwa ufanisi endapo hakutakuwa na mgawanyiko nchini kama ambavyo ilivyo sasa.

Ameeleza, Serikali inatambua kuwa kuna tofauti nyingi nchini ikiwemo za makabila na madhehebu lakini tunu inayounganisha watu wote ni haki, uhuru, umoja na amani ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia nchi.


"Mheshimiwa Rais anatambua kutofautiana ikiwemo katika mawazo lakini kama mnavyojua kuwa amekuwa ni muumini wa maridhiano kwani anayaishi na anatoa nafasi kwa kila mmoja kutoa mawazo yake bila kubughudhiwa."
Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amemtakia kila la heri Askofu Mwijage katika majukumu yake mapya kwenye kanisa na malezi ya jamii kwa ujumla na kueleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa imani kuwa ni kiini cha ustaarabu na uungwana miongoni mwa jamii.

Ameongeza kuwa, kuwekwa wakfu kwa Askofu Mwijage kunatoa mafundisho
mengi ikiwemo kutotanguliza hofu pale kunapotokea majukumu mapya
kutokana na Askofu huyo kuwa tayari kutumikia majukumu yake bila kuweka vikwazo mbele na kwamba hili ni somo kwa wananchi wengine kuwa
tayari kutekeleza majukumu bila kutanguliza vikwazo.

Wakati huohuo, Dkt.Biteko amempongeza aliyekuwa Askofu Msaidizi wa
Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Askofu Methodious Kilaini ambaye leo ametangaza kustaafu rasmi na kumueleza kuwa, Serikali inatambua mchango wake na kwamba asisite kutoa mawazo yake katika kujenga nchi
na ustawi wa jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa Katoliki mkoani humo nia ikiwa ni kuchagiza maendeleo na amani mkoani Kagera.

Amempongeza Askofu Mpya, Mhashamu Jovitus Mwijage kwa kuwekwa Wakfu
huo na kumtakia kila la heri katika majukumu yake mapya katika kukuza
imani na masuala mengine yanayohusu jamii.

Aidha, ametoa pongezi kwa Askofu Mstaafu, Mhashamu Desderius Rwoma kwa
utumishi wake uliotukuka na kueleza kuwa Mkoa wa Kagera unatambua
mchango wake katika ustawi wa Mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Flavian Kasala amesema kuwa, kuwekwa wakfu kwa Askofu huyo mpya wa Jimbo la Bukoba kumefanya majimbo yote yapatayo 35 nchini kuwa
na Wachungaji Wakuu ambao ni Maaskofu na amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuendelea kusimamia ipasavyo Kanisa Katoliki duniani.

Amempongeza Askofu Mstaafu wa Jimbo hilo, Mhashamu Desiderius Rwoma (2013-2022) kwa kuliongoza Jimbo hilo katika kipindi chote na kueneza
injili katika Jimbo la Bukoba.

Pia, amemshukuru Dkt. Doto Biteko kwa kuhudhuria sherehe hizo na hii ikionesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na madhehebu mbalimbali nchini.


No comments:

Post a Comment