TAMISEMI,UNICEF WATETA AFYA YA MSINGI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 19, 2024

TAMISEMI,UNICEF WATETA AFYA YA MSINGI


Na. Asila Twaha, OR- TAMISEMI

Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume Januari 18, 2024 amekutana na kuzungumza na Wadau wa Shirika la UNICEF.

Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Idara ya Afya- TAMISEMI Dodoma kikiwa na lengo la kujadiliana jinsi ya kuimarisha utekelezaji wa vipaumbele vya Sekta ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe vinavyotekelezwa kwa ushirikiano na UNICEF.


Pia majadiliano hayo yalilenga UNICEF kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendelea kuboresha Mifumo ya sekta ya Afya nchini hasa katika ngazi ya Huduma ya Afya ya Msingi.

Dkt. Mfaume amesema, Serikali inaendelea kuboresha Mifumo Stahimilivu ya sekta ya Afya na kwamba Ofisi ya Rais - TAMISEMI inalo jukumu la Kuratibu Utekelezaji wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na itahakikisha huduma bora kwa wananchi zinatolewa wakati wote katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ngazi ya Msingi.

" Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa katika ngazi ya huduma za Afya ya Msingi" amesema Dkt. Mfaume

Naye Mkuu wa Seksheni ya Afya Shirika la UNICEF Bi. Wendy Erasmaus amesema, sekta ya Afya ni muhimu sana kwa wananchi na Shirika hilo linafurahi kufanya kazi na kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuendelea kuchangia utatuzi wa changamoto za sekta ya Afya, kuweka na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watanzania.

" Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais- TAMISEMI katika kutekeleza afua katika ngazi ya Huduma ya Afya ya Msingi" amesema Bi.Wendy

Kikao hicho kiliwashirikisha watalaamu kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais - TAMISEMI.

No comments:

Post a Comment