NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uraribu Mhe. Jenista Mhagama ameagiza kurejeshwa kwa huduma zote za kijamii zilizoharibiwa na maji ya mvua kubwa iliyonyesha Januari 25 2024 Manispaa ya Morogoro na kusababisha watu zaidi ya 200 kukosa makazi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kina juu ya madhara yaliyojitokeza ili kuja na takwimu sahihi za idadi ya waathirika na uhalibifu kwa maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua hizo.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuzitaka Taasisi zote zinazohusika kuchukua hatua za haraka ikiwemo TANESCO, TARURA na TANROADS ili kuendelea kurejesha hali ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua hizo mkoani Morogoro.
Aliongezea kuwa, kila taasisi ifanye kazi usiku na mchana ili kusaidia kurejesha miundombinu ikiwemo barabara zilizoathiriwa na mvua hizo.
“Ni wakati wa kufanya kazi usiku na mchana, Serikali hailali hasa katika maafa ya namna hii, Hongereni TANESCO kwa kurejesha miundombinu ya umeme kwa haraka hii inafaa kuingwa na wengine pia, tutaendelea kushirikiana na mkoa katika hatua zote muhimu,” alisisitiza Mhe. Mhagama
Sambamba na hilo alitoa wito kwa jamii kuendelea kuchukua hatua za tahadhari kwa kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka husikia ikiwemo za utabiri wa hali ya hewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima alimshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo yake na namna Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa wanavyoendelea kutoa ushirikiano kwa mkoa kuhakikisha hali inarejea na kuwaasa wananchi kuwa watulivu katika kipindi hicho.
“Wananchi endeleeni kutoa ushirikiano kwa serikali huku mkiwa katika utulivu kwa kuzingatia mvua hizi ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi hivyo katika mkoa wetu hatujawahi pata mvua za aina hii, na sisi kama Mkoa hatuta lala ili kuhakikisha mnaendelea kuwa salama pamoja na mali zenu,” alieleza Mhe. Malima
No comments:
Post a Comment