Na Carlos Claudio, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imefanya uzinduzi wa vifaa vya TEHAMA na kukabidhi magari kwa halmashauri 13 pamoja na kufanya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa utumishi wanaoshughulikia changamoto za upandaji wa madaraja ya walimu.
Pia imewatangazia maafisa wote kuhakikisha walimu wote wanatekelezewa majukumu yao vyema ili kurekebisha kasoro zilizokuwepo na kuwaweka walimu wote nchini katika usawa.
Akizungumza Januari 3,2024 jijini Dodoma, Waziri wa nchi, ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema walimu wote nchini ambao wapo katika vitongoji, vijijini, kata, tarafa, halmashauri, wilaya, mikoa, wizarani waweze kutekelezewa majukumu yao vyema.
“Maelekezo yangu hata walimu ambao wapo kitandani leo hii, pengine wana madhira mbalimbali ya ugonjwa, wapo mahospitalini, wenye dharura za ugonjwa haki zao zishughulikiwe mara moja ili tuweze kurekebisha kasoro zilizokuwepo na kuwaweka walimu wote nchini katika usawa kama ndoto za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hasan anavyosisitiza wakati wote kwa walimu wote nchini,” amesema Mhe Mchengerwa
Amesema pamoja na walimu kupata haki zao wapo wakurugenzi wa halmashauri baadhi yao hawajalipa stahiki maafisa utumishi ambao wamekuja Dodoma kufanya zoezi hilo la ufunguzi wa kikao hiko cha maafisa utumishi pamoja na uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya TEHAMA na amesisitiza kuwa mpaka itakapofika Jumatatu kuwa wakurugenzi wote nchini wawe wamewalipa maafisa utumishi posho zao.
Ameagiza waajiri pamoja na mamlaka zote zinazohudumia walimu wasimamie vyema maslahi ya walimu ndani ya siku 14 ili kutatua changamoto na kero zinazowakabili walimu hao.
“Niweke wazi, mimi sitamvumilia mtendaji yoyote ambaye hawajibiki kushughulikia kero za walimu na vilevile sitamani kusikia walimu wanalalamika kuhusu maslahi yao ya kiutumishi wakati huu ambao Mhe. Rais ameridhia na kunipa heshima ya kuwa waziri katika sekta hii eneo hili la TAMISEMI”.
Amesema wakuu wa divisheni ya awali na msingi katika halmashauri 13 wanaenda kupewa magari yaliyo nunuliwa kupitia mfuko wa ushirika wa kusaidia maendeleo ya elimu Global Partnership in Education (GPE) kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8.
Serilkali ilisaini mradi mpya na GPE unaofahamika kama Teachers Support Programme ambao afua zake zinajikita kuboresha mazingira ya walimu nchini na utekelezaji wa mradi huo ambao umeanza mwaka wa fedha 23/24 na mradi wote unagharimu jumla ya dola milioni 105 laki 8.31 ambao ni sawa na shilingi bilioni 264.
Amesema Rais kwa mara ya kwanza ameweza kununua magari 432 na kugawa kwa maafisa elimu msingi na sekondari wa nchi nzima sambamba na awali alivyowagusa wasimamizi katika sekta ya afya kwani kwa kufanya hivyo TAMISEMI elimu na sekta ya afya ina watendaji kiajira wanatengeneza idadi ya watumishi wa umma zaidi ya asilimia 70.
Naye mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya TAMISEM Mhe. Denis Londo amesema uwekezaji mkubwa umefanywa na bila shaka vifaa ambavyo vinakabidhiwa vinaenda kuleta tija na kuongeza uelewa kwa wanafunzi pamoja na kuleta mazingira rafiki kwa watumishi wa idara ya elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema mkoa unahakikisha wanafunzi wanaripoti shuleni na hali ya kuripoti kwa sasa kwa shule za awali mkoa umefikisha asilimia 92, kwa darasa la kwanza umefikisha asilimia 95 na kwa kidato cha kwanza umefikishaa asilimia 97 mpaka jana Ijumaa tarehe 2 Februari.
Amesema mkoa wa Dodoma umepokea magari pamoja na vifaa vya TEHAMA na ana ahidi kuvitunza na vitatumiwa kwa makusudi na fadhila iliyokusudiwa ili viweze kuleta tija katika sekta ya elimu mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment