Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), imesema zoezi la kuondoa vibanda vilivyojengwa kwenye eneo la hifadhi ya Barabara kwa Barabara kuu za mkoa wa Tanga, linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 inayopiga marufuku uwekaji wa miundombinu yoyote kwenye eneo hilo bila idhini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mhe. Paul Mnzava aliyeuliza Je lini Serikali itaacha kuwafukuza na kuwavunjia vibanda Wajasiriamali wanaofanya biashara Barabara Kuu ya Segera – Korogwe – Moshi.
Eng. Kasekenya amesema TANROADS ilibomoa vibanda vya Wafanyabiashara ambavyo havikupangwa kwa mpangilio mzuri na vibanda vilivyopangwa kwa mpangilio havikubomolewa.
Aidha, Mbunge wa Busega Simon Lusengekile alitaka kujua Je lini Barabara ya Nyashimo – Ndutwa – Shigala – Malili hadi Ngasamo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Akijibu swali hilo, Eng. Kasekenya amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) tayari imekamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Nyashimo - Ndutwa – Shigala – Malili hadi Ngasamo (km 48).
Eng. Kasekenya amesema Mkataba wa Mhandisi Mshauri unatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi Februari 2024 na kazi ya usanifu inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2024. Baada ya kazi hiyo kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga Barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
No comments:
Post a Comment