Msanii wa Mali na Ufaransa Nakumura |
Kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Paris ilisema imeshangazwa na mashambulizi ya "kibaguzi" yaliyofanywa na makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia ya Ufaransa dhidi ya mwimbaji wa Mali na Ufaransa Aya Nakamura.
Mashambulizi hayo yalichochewa na ripoti kwamba Nakamura, 28, angeimba wimbo wa mwimbaji mashuhuri wa Ufaransa wa karne ya 20 Édith Piaf katika sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris mnamo Julai.
Siku ya Jumapili, kundi la siasa kali za mrengo wa kulia la Les Natifs liliandamana mjini Paris na bango lililosema: "Hakuna njia Aya, hii ni Paris, si soko la Bamako", ikimaanisha mji mkuu wa Mali, ambako Nakamura alizaliwa.
Alihamia Ufaransa na familia yake akiwa mtoto na akapokea uraia wa Ufaransa mnamo 2021.
Nyota huyo wa muziki pia alizomewa na wafuasi wa chama cha mrengo wa kulia cha Reconquest wakati wa mkutano uliofanyika Jumapili.
“Tumeshtushwa sana na mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya Aya Nakamura katika siku za hivi majuzi. [Tunatoa] usaidizi wetu kamili kwa msanii huyu wa Ufaransa anayesikilizwa zaidi duniani,” kamati ya maandalizi ya Olimpiki ya Paris ilisema Jumatatu.
Mashabiki kadhaa na viongozi wa Ufaransa, akiwemo Mbunge wa Ufaransa Antoine Leaument na Waziri wa Michezo Amelie Oudea-Castera, wamemuunga mkono Nakamura.
Les Natifs imeendelea kumbagua msanii huyo , likisema Nakamura hawakilishi utamaduni wa Ufaransa na utendaji wake utaashiria "Uafrika" wa utamaduni wa Kifaransa.
Nakamura ni mmoja wa wanamuziki wakubwa nchini Ufaransa, na baadhi ya ripoti zinamtaja kuwa mwanamuziki anayeimba Kifaransa anayesikilizwa zaidi duniani.
No comments:
Post a Comment