Maono ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Kitaifa kama Ujenzi wa Bwawa la Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kama vile Daraja la Kigongo - Busisi yametekelezwa na yanaendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika Misa Takatifu ya kumuombea Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Wilayani Chato Mkoani Geita.
“Niwahakikishie Watanzaniza kuwa miradi yote ambayo Hayati Dkt. Magufuli akiwa Rais wa Nchi yetu, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaiendeleza yote kwa kasi kubwa ili tumuenzi kwa vitendo”, amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa Watanzania watamkumbuka Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwezo wake wa kiuongozi, karama yake ya kutatua changamoto za wananchi pamoja na kuwasikiliza, kuondoa kero mahali penye kero, kuhimiza uwajibikaji Serikalini kwa kuondoa uzembe, ubadhirifu na rushwa.
Katika Misa hiyo, Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa jipya la Mtakatifu Yohana Maria Muzeyina na kuweza kukusanya takribani Milioni 169 pamoja na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa nafasi ya Uwaziri katika Wizara ya Ujenzi ambayo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alihudumia miaka 20.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shingella amemshukuru Rais Samia kwa kutimiza ndoto za Hayati Magufuli za kujenga barabara kuunganisha Mkoa wa Geita na Shinyanga kwa kiwango cha lami ambapo tayari Serikali imesaini mtakataba wa ujenzi kilometa 73 kwa kiwango cha lami kuanzia Kahama hadi Kakola.
Kwa niaba ya Famia ya Hayati Magufuli, Jesca Magufuli, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa karibu na familia kuwafariji, kuwajali na kuwapatia matunzo yote kadri awezavyo.
Jesca ameongeza kuwa kama familia wataendelea kumuenzi na kumkumbuka Hayati Dkt. Magufuli kwa namna alivyowapenda na kuwawekea misingi mizuri ya kuchapa kazi na kumtanguliza Mungu mbele kwenye kila jambo.
Misa ya Kumbukizi ya Miaka Mitatu tangu alipofariki Hayati Dkt. John Pombe Magufuli imeongozwa na Makamu Askofu, Padri Ovan Mwenge na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM), ndugu, jamaa na marafiki.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi
No comments:
Post a Comment