PAC YAKAGUA MRADI WA UBORESHAJI KIWANJA CHA NDEGE TABORA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, March 17, 2024

PAC YAKAGUA MRADI WA UBORESHAJI KIWANJA CHA NDEGE TABORA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetembelea na kukagua mradi wa ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha ndege cha Tabora unaotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Kamati hiyo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Japhet Hasunga (Mb), ikiwa mkoani Tabora Machi 17, 2024 imeshauri kwa Wakala huo masuala mbalimbali ikiwemo kumsimamia Mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili wananchi wa Tabora na mikoa jirani waweze kunfaika na mradi huo.

"Msimamieni Mkandarasi aongeze kasi ya utekezaji wa mradi ili ukamilike kwa wakati, nao wananchi wa Tabora na mikoa jirani waweze kufurahia huduma ya usafiri wa anga", amesema Hasunga.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Ludovick Nduhiye amesema Wizara imepokea ushauri na maelekezo ya Kamati na kuahidi kuyafanyia kazi kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema Mradi huo umefikia asilimia 38 na unahusisha Ujenzi wa Jengo la abiria litakalohudumia abiria 120 kwa wakati mmoja, Mnara wa kuongoza ndege, barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani pamoja na ujenzi wa uzio wa usalama wenye urefu wa kilometa 6.25

Mradi wa Uboreshaji na Ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora utagharimu Tsh. Bil. 24 na unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Oktoba 2024.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi. 



No comments:

Post a Comment