Achana na mechi ya Dar Es Salaam Derby kati ya Azam na Yanga itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga kwa sasa inawaza zaidi mechi mbili za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakapocheza na wakali Mamelodi Sundowns kutoka Afrika kusini, ikianzia kwa Mkapa Machi 30 kisha kurudiana Kwa Madiba, Aprili 6.
Mechi hiyo kwenye makaratasi inaonekana kuwa ngumu kwa Yanga. Hiyo ni kutokana na bora wa Mamelodi ya sasa lakini, Wasauzi hao kuwa mbali katika uwekezaji ukilinganisha na Wanajangwani lakini uhalisia huenda ikawa mechi dume kwa pande zote mbili.
Yanga ya sasa pia imejipata. Uwanjani ina mastaa kibao ambao wanaweza kufanya lolote muda wowote na kwa mtu yeyote, hivyo mechi na Mamelodi zitaamuliwa na dakika 180 za uwanjani.
Ukiachana na hayo, kikosini kwa Yanga kuna silaha tatu muhimu ambazo zinaijua vyema Mamelodi na kama Wananchi watazitumia vyema basi zitaleta matokeo chanya kwa kuivusha salama mbele ya wapinzani wao ambao juzi usiku walituma mashushushu kuisoma Yanga ilipokuwa ikivaana na Geita Gold katika mechi ya Ligi Kuu.
Miguel Gamondi Kocha mkuu Yanga SC. |
GAMONDI
Huyu ndiye mkuu wa benchi la ufundi la Yanga. Muargentina huyu ndiye anafanya uamuzi wa nani acheze, nani asicheze, timu icheze kwa mfumo upi na mbinu zipi na mambo mengine yote ya kiufundi inayoogopwa na wengi kwa sasa Afrika.
Mkali huyu mwaka 2005 hadi 2006, alikuwa kocha mkuu wa Mamelodi na kuwawezesha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo ambao walikuwa wameumisi' kwa kipindi cha miaka sita.
Kukaa kwake Mamelodi ni silaha tosha, lakini pia mwenyewe alipoulizwa baada ya kupangwa na timu hiyo alikiri timu hiyo ina uwekezaji mkubwa lakini
anaamini Yanga yake inaweza kutoboa.
"'Naijua Mamelodi. Kuna utofauti wa vitu vingi na hapa Yanga lakini nachoamini soka huchezwa na watu 11 dhidi ya 11 uwanjani, Itakuwa mechi ngumu lakini naamini tuna timu ya kuweza kupambana nao na kuleta matokeo chanya," alisema Gamondi.
Skudu Makudubela mchezaji wa Yanga SC. |
SKUDU
Soka ni zaidi ya kucheza uwanjani hususani mpira wetu wa Afrika umegubikwa na vitu vingi ndani na nje hii ni silaha nyingine kwa Yanga dhidi ya Mamelodi.
Licha ya Kwamba Skudu nafasi yake ya kucheza kikosini Yanga ni finyu lakini anamchango mkubwa
katika mechi dhidi ya Mamelodi.
Mwamba huyu kabla ya kutua Yanga mwanzoni mwa msimu huu, Maisha yake yote ya Soka aliyafanya akiwa kwao Afrika kusini, amecheza Ligi Ku nchini humo kwa zaidi ya miaka 10 na timu tofauti na kukutana na Mamelodi mara kadhaa. Lakini pia Skudu alipita kwenye akademi ya Mamelodi mwaka 2012, hivyo baadhi ya maisha ya Masandawana anayajua.
Kama Yanga itamtumia vyema Skudu kwenye kupata baadhi ya taarifa za wachezaji atawasaidia, lakini pia uzoefu wake na aina ya soka la Afrika kusini vitawasaidia pia. Baada ya kupangwa na Mamelodi, Skudu alisema: "Ni timu nzuri na bora tumepangwa nayo, tunatakiwa kushinda ili kusonga mbele na tuko tayari kufanya hivyo."
Mpho Maruping Mtaalamu wa kusoma video za wapinzani Yanga SC. |
MARUPING
Unamjua huyu ni nani? Kama haujui basi tambua ni mtathmini mchezo wa Yanga (Video Analyst) raia wa Afrika Kusini, jina lake kamili ni Mpho Maruping.
Huyu ndiye yupo nyuma wa zile mbinu, za Gamondi, maufundi ya Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki
sambamba na ubabe wa Kharid Aucho katikati ya uwanja.
Kazi yake mama ni kuwasoma wapinzani na kujua wananguvu gani, kwenye eneo lipi, wapi ni hatari na
wapi wanavuja lakini pia kuonyesha uhatari wa mpinzani ni wa aina gani na wachezaji gani hutumika.
Akishafanya hivyo hukabidhi ripoti kwa benchi la ufundi na kulifanyia kazi hivyo ndio maana unaona Yanga ya msimu huu karibu mechi zote ilizocheza ime mudu mpinzani.
Ukiachana na kazi zake hizo, Maruping anaijua vyema Mamelodi ndani na nje ya uwanja. Amewahi kucheza nao kipindi ni mchezaji kabla ya kustaafu na kugeukika ukocha na kazi hiyo anayoifanya sasa Yanga.
Mtaalamu huyo amefanya kazi hiyo akiwa na timu mbalimbali za Afrika Kusini sambamba na ile ya taifa ya wanawake "'Banyana Banyana'. Kubwa zaidi Maruping amefanya kazi kwenye Akademi ya soka ya wanawake 'Banyana Banyana'. Kubwa zaidi Maruping amefanya kazi kwenye Akademi ya soka ya Venda inayomilikiwa na Rais a sasa wa CAF, Patrice Motsepe ambaye aliwahi kuwa mmiliki wa Mamelodi kabla ya kumuachia timu hiyo mwanaye aitwaye Thopie Motsepe.
Ukiunganisha doti vizuri utaelewa namna Maruping anavyoijua vyema Mamelodi nje ndani.
No comments:
Post a Comment