U.S. CDC NA THPS WAKABIDHI VIFAA NA JENGO JIPYA LA TIBA NA MATUNZO KWA WAVIU USHETU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 16, 2024

U.S. CDC NA THPS WAKABIDHI VIFAA NA JENGO JIPYA LA TIBA NA MATUNZO KWA WAVIU USHETU

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed Kabojela (katikati),Mkuu wa Tawi la Huduma za Kliniki kutoka U.S.CDC Tanzania, Dkt. Daniel Magesa (kushoto) na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa THPS akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa THPS Bw. George Anatory wakikata utepe wakati THPS ikikabidhi jengo la kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU) katika kituo cha Afya Bulungwa

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) limekabidhi jengo la kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU) pamoja na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi Milioni 768.2 katika Kituo cha Afya Bulungwa kilichopo Kata ya Bulungwa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.

Hafla ya makabidhiano imefanyika Ijumaa Machi 15,2024 katika viwanja vya kituo cha Afya Bulungwa ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed Kabojela na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi jengo na vifaa hivyo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa THPS, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa THPS Bw. George Anatory amesema THPS imekabidhi jengo hilo la CTC baada ya kukamilisha ukarabati wa Kituo cha tiba na matunzo ya Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) Kituo cha Afya Bulungwa.
Muonekano sehemu ya jengo jipya la CTC kituo cha Afya Bulungwa halmashauri ya wilaya ya Ushetu.

Ameeleza kuwa, zoezi la ukarabati wa jengo hilo umegharimu jumla ya TZS. 204,468,950 (USD M81,787.58) ikiwa ni sehemu ya mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na THPS kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S CDC).

“Kituo kimeimarishwa ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi katika Wilaya ya Ushetu wanapata huduma bora za afya na matibabu na hii ni pamoja na kubomoa jengo, uashi, vyuma, kuezeka paa, mfumo wa kutupa maji ya mvua, milango na madirisha, finishes, samani, usafi wa mitambo, usambazaji wa maji. mabomba, mifereji ya maji taka na mfumo wa uingizaji hewa, vifaa vya mabomba na mfumo wa umeme”,amesema Anatory.

Amefafanua kuwa, ukarabati wa jengo na manunuzi ya vifaa vote vya kutolea huduma za afya yamefadhiliwa na CDC kwa ufadhili wa PEPFAR hivyo kusisitiza umuhimu wa matumizi sahihi na matengenezo ya vifaa hivyo ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora za tiba na matunzo ya VVU sambamba na kuhimiza ufuasi wa huduma za tiba ya ARV kwa wapokea huduma.

“Tunakabidhi jengo la kutolea huduma za tiba na matunzo kwa Watu wanaoishi na VVU (WAVIU) pamoja na Samani (Furniture ) ziikiwemo Meza 122, Viti 231, Kabati 92), Vitendea kazi (zikiwemo Friji 45, Printa 5), na vifaa tiba za tiba mgandisho (5) kwa ajili ya matibabu ya dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi (Cryotherapy Machine). Vifaa vyote na Jengo vimegharimu jumla ya Shilingi 768,220,190”,ameongeza Anatory.
Muonekano wa sehemu ya vifaa mbalimbali kwa ajili ya vituo vya afya katika halmashauri ya Ushetu vilivyotolewa na shirika la THPS

“Nina imani kuwa msaada tuliotoa utaboresha utoaji wa huduma za kinga, tiba na matunzo ya VVU, na kusaidia kuokoa maisha katika wilaya ya Ushetu na maeneo jirani. THPS inaahidi kuendelea kushirikiana na Timu za usimamizi wa shughuli za huduma za afya kwa ngazi ya Mkoa na Halmashauri zake kuhakikisha malengo ya Serikali ya kutokomeza VVU na UKIMWI lifikiwe”,amesema Anatory.

Aidha Anatory amesema shirika lake limejipanga kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha watanzania wote wanapata huduma bora za afya na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Tawi la Huduma za Kliniki kutoka U.S.CDC Tanzania, Dkt. Daniel Magesa, ameeleza kuwa, serikali ya Marekani inaitambua na kuipongeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI), viongozi wa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia kwa dhamira ya kuboresha matokeo ya afya nchini Tanzania.

Amesisitiza kuwa, kuongezeka kwa ushirikiano katika kinga, tiba na matunzo ya VVU na UKIMWI kutasaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya na VVU ambapo Serikali ya Marekani inatambua na kuunga mkono ahadi hiyo.

Dkt. Magesa amesema Kituo hicho kipya cha Tiba na Matunzo kwa WAVIU kilichokarabatiwa kinatarajiwa kuweka mazingira bora ya kutoa huduma za tiba na matunzo ya VVU na hivyo kusababisha ongezeko la watu wanaopata huduma katika kituo hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed Kabojela.

Kwa upande wake mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed Kabojela, ametoa shukrani zake kwa msaada mkubwa uliotolewa na serikali ya Marekani kupitia THPS katika kudhibiti janga la UKIMWI na kuokoa maisha ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.

Amesema jengo hilo na vifaa vilivyotolewa vitaboresha Huduma za Afya katika Halmashauri ya Ushetu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla, pia mazingira hayo kwa sasa yatakuwa rafiki kwa watoa huduma za afya na yataongeza ari kwa watumishi katika kutoa huduma za afya.

“Serikali yetu, kwa kushirikiana na wenzetu wa CDC kupitia THPS, imeweka nguvu kubwa sana kwenye mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kutumia mbinu mbalimbali. Lengo ni kudhibiti maambukizi mapya, kuibua wote wenye maambukizi na kuwapatia matibabu waimarike afya na wafikie kiwango cha kufubaza virusi ili waweze kuishi maisha yao ya kawaida na kushiriki kujenga uchumi wa Taifa letu. Tutaendelea kudumisha ushirikiano unaohitajika na CDC na THPS ili kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI”,amesema Kabojela.
“Kwa namna ya pekee naomba nitoe Shukrani za dhati kwa taasisi ya THPS kwa kuona mapungufu yaliyokuwepo katika jengo hili na kuamua kuyarekebisha. Nawahakikishia kuwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga utasimama kidete kuhakikisha jengo hili linaendelea kuwa nadhifu na kutumika sawa na makusudio yake ya kutolea huduma jumuishi za VVU. Tunaishukuru sana PEPFAR na US CDC kwa ufadhili huu adhimu utakaosaidia kuongeza ufanisi katika kutoa huduma za tiba na matunzo kwa WAVIU”,ameongeza Kabojela.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Gagi Lala ameishukuru THPS na CDC kupitia PEPFAR kwa kujenga jengo la kisasa kwa ajili ya huduma za tiba na matunzo katika kituo cha Afya Bulungwa huku akiomba CTC nyingi zaidi zijengwe kwani mahitaji ni makubwa katika halmashauri hiyo yenye kata 20 lakini kuna CTC 10 tu.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Bulungwa Dkt. Maziku Ngusa amesema kituo hicho kilianza kutoa huduma za tiba na matunzo mwaka 2007 wakiwa na chumba kimoja pekee ambapo kupatikana kwa kituo kipya kunaweka mazingira rafiki ya utoaji huduma ikiwemo kuongeza usiri mkubwa kwa wateja.

Mratibu wa Kudhibiti wa Kudhibiti UKIMWI Mkoa wa Shinyanga Dkt. Peter Mlacha amesema mkoa wa Shinyanga unatoa huduma za tiba za matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU 79,126 ambapo hadi februai 29, 2024, Halmashauri ya Ushetu ina jumla ya vituo 10 vya kutolea huduma za tiba na matunzo ikihudumia WAVIU zaidi ya 12,140 waliosajiliwa katika kliniki 20 za tiba na matunzo kwa WAVIU.

KUHUSU THPS

Tanzania Health Promotion Support (THPS) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2011, ambapo kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (US. CDC) , THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU/UKIMWI; Kifua kikuu; kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto; huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa afya, na UVIKO-19.


Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021- Septemba, 2026), unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya (Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga) na katika jamii (Kigoma, Pwani na Tanga). Huduma hizi ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wasichana balehe na wanawake wadogo katika mkoa wa Shinyanga.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed Kabojela akizungumza Ijumaa Machi 15,2024 wakati wa hafla ya kukabidhi jengo la kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU) katika kituo cha Afya Bulungwa na vifaa mbalimbali kutoka shirika la THPS kwa halmashauri ya wilaya ya Ushetu Mkoa wa Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed Kabojela akionesha cheti cha shukrani kutoka Halmashauri hiyo kwa shirika la THPS kuhusu Mapambano dhidi ya VVU.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Mohamed Kabojela akimkabidhi Mkurugenzi wa Uendeshaji wa THPS aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa THPS Bw. George Anatory cheti cha shukrani kutoka Halmashauri hiyo kwa shirika la THPS kuhusu Mapambano dhidi ya VVU.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa THPS akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa THPS Bw. George Anatory akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi jengo la kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU) katika kituo cha Afya Bulungwa na vifaa mbalimbali kutoka shirika la THPS kwa halmashauri ya wilaya ya Ushetu Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa Tawi la Huduma za Kliniki kutoka U.S.CDC Tanzania, Dkt. Daniel Magesa akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi jengo la kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU) katika kituo cha Afya Bulungwa na vifaa mbalimbali kutoka shirika la THPS kwa halmashauri ya wilaya ya Ushetu Mkoa wa Shinyanga.
Mratibu wa Kudhibiti wa Kudhibiti UKIMWI Mkoa wa Shinyanga Dkt. Peter Mlacha akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi jengo la kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU) katika kituo cha Afya Bulungwa na vifaa mbalimbali kutoka shirika la THPS kwa halmashauri ya wilaya ya Ushetu Mkoa wa Shinyanga.

No comments:

Post a Comment