WAFUGAJI nchini bado wanakabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo sheria kandamizi, uhaba wa malisho na migogoro baina yao na wakulima hali ambayo imekuwa ikisababisha mapigano kati ya jamii hizo mbili na kusababisha vifo imeelezwa.
Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Taifa Mhandisi Simon Ndaki, alibainisha hayo jijini Dodoma, alipokuwa akieleza vipambele vyake atakavyo vifanyia kazi mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania kiti hicho.
Amesema, wafugaji nchini bado wanakabiliwa na kero mbalimbali ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ili mifugo iwe na tija nchini.
"Wafugaji nchini bado wanachangamoto nyingi mimi kama nitachaguliwa kwenye uchaguzi huu wa CCWT nitahakikisha nashirikiana na serikali kuzifanyia kazi ili ufugaji nchini uwe na tija kwa wafugaji na Taifa"amesema
Amesema kero nyingine atakayo ifanyia kazi ni sheria kandamizi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ili kuondoa hali iloyopo hivi sasa ya kuwanyonya wafugaji.
"Zipo sheria hii leo mfugaji kama mfugo wake utakamatwa basi anatozwa faini ya shilingi 100,000 kwa kila kichwa cha ng’ombe hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuwafilisi wafugaji"amesema Ndaki
Aidha, amesema kero nyingine ni ukosefu wa masoko ya uhakika ya bidhaa za mifugo nchini hali ambayo imekuwa ikichangia wafugaji kuendelea kuwa maskini.
"Kama nitachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hichi nitakifanya kuwa taasisi siyo chama cha wanaharakati lakini katika hii kero ya masoko nitahakikisha kuwa wafugaji wanauza mifugo yao kwa kilo siyo kwa macho kama ilivyo sasa"amesisitiza
Pia, amesema kama atapata nafasi hiyo atahakikisha anashirikiana na serikali kukomesha mauaji ya wafugaji yanayotokana na askari wa mapori ya hifadhi ya misitu kuwapiga risasi wanapo ingiza mifugo yao hifadhini.
"Lakini pia nitahakikisha kuwa mifugo yetu inakuwa na tija na kusaidi katika kuchangia kwenye pato la taifa kama ilivyo Botuswana yenye mifugo michache ukilinganisha na Tanzania"alisema
Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi wa Chama cha Wafugaji CCWT, Charles Malagwa alisema hivi sasa wagombea mbalimbali wanachukua fomu kwa ajili ya uchaguzi ngazi ya taifa utakaofanyika Aprili 8, mwaka huu.
"Nitoe rai kwa wagombe wote kuhakikisha kuwa wanafanya kampeni zao kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi utakao fanyika Aprili 8, mwaka huu na atakaye kiuka rungu la tume litamshukia"amesisitiza Malagwa
No comments:
Post a Comment