SERIKALI KUPITIA TANROADS YAKUSUDIA KUTEKELEZA MIRADI 7 YA KIMKAKATI YA UJENZI WA BARABARA NA MADARAJA GEITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 20, 2024

SERIKALI KUPITIA TANROADS YAKUSUDIA KUTEKELEZA MIRADI 7 YA KIMKAKATI YA UJENZI WA BARABARA NA MADARAJA GEITA


Serikali ya awamu ya sita kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekusudia kutekeleza miradi saba ya kimkakati ya Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Mkoani Geita baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo tarehe 12 Machi 2024; Meneja wa TANROADS Mkoani Geita Mha. Ezra Daniel ametaja miradi ambayo Serikali imekusudia kuijenga ni ujenzi wa barabara ya Geita - Nzera - Nyamadoke (km 50), Mtakuja - Buhalahala (Geita mjini) Km 24, Nyankumbu - Nyang’wale/Busolwa - Kharumwa - Nyang’holong hadi kahama (Km 162),

Ujenzi wa barabara ya Kashelo - ilolangulu/Ishigamva - Ushirombo (km 30), Nyamirembe port - Katoke (Km 51), Katoro - Ushirombo(Km 59) na Mtakuja - Bukoli - Buyange - Kahama ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 tayari Serikali imeshatenga fedha ili barabara ziweze kutangazwa kumpata mkandarasi ambaye ataanza kazi ya ujenzi.


Amesema lengo la Serikali ni kujenga barabara kila Wilaya Mkoani Geita ikiwemo kufanya stadi ya kuweza kuijenga barabara ya njia nne Geita mjini ili kuweza kurahisisha usafirishaji wa Wafanyabiashara wa madini kutoka Geita na kwenda kuuza Nchi jirani kupitia Miundombinu bora ya barabara.

Amesema zaidi ya taa za barabarani 300 zimewekwa kwenye takribani kilometa 5 katika mji wa Geita na Katoro, na katika mwaka wa fedha 2023/24 wamepanga kuweka taa 120 katika mji wa Runzewe.

"Hali ya mtandao wa barabara ni nzuri kwa sababu zinapitika zote kwa mwaka mzima katika majira yote, hatuna Sehemu ambazo barabara yetu imejifunga na katika hali hii ya mvua za El - nino tunashukuru haijaleta madhara mkoani Geita” amesema Mha. Daniel

Naye Mkurugenzi wa Matengenezo kutoka TANROADS Mkoa wa Geita, Mha. Fredrick Mande ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita katika kipindi cha miaka 3 kwa kuendelea kutoa fedha ambazo zimetumika na zinaendelea kutumika kwa ajili ya kazi ya matengenezo ili kunusuru hali ya barabara zisijifunge.

Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na Mikoa jirani kuweza kutunza taa, alama za barabarani pamoja na kutokuvamia hifadhi za barabara na kutozidisha mizigo/uzito wa magari barabarani ili kuweza kuzilinda ziweze kutumika muda mrefu.

Aidh Mkoa wa Geita, unahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1019.13, ikiwa barabara kuu ni kilometa 236.18 na barabara za Mkoa ni kilometa 704, pamoja na jumla ya madaraja na makalvati 305.

No comments:

Post a Comment