Angela Msimbira GEITA
KAMATI ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (LAAC) imetoa miezi 3 kwa Halmashauri ya Mji wa Geita kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Bulela kilichopo katika Kata ya Bulela mkoani Geita.
Agizo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mheshimiwa Staslaus Mabula wakati wa majumuisho ya ziara ya Kamati ya LAAC ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Geita, mkoani Geita.
Amesema kuwa kituo hicho kitaendelea kutoa huduma huku kikiendelea kufanyiwa marekebisho mbalimbali ikiwemo kubadilisha sakafu na milango ambayo haina ubora.
Mabula pia ameishauri Halmashauri hiyo kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba ili kituo hicho kinapokamilika kiweze kuwa na vifaa vitakavyoweza kutoa huduma bora kwa jamii
Pia imependekeza chumba cha upasuaji kikamilishwe kwa wakati na kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa vifaa ili kuanza kutoa huduma za upasuaji kwa mama wajawazito.
"Chumba cha upasuaji ni eneo muhimu sana kwa kuwa huko ndipo tunapowalenga wamama wajawazito wenye changamoto kupata matibabu hivyo hakikisheni inakamilika na vifaa vinakuwepo," amesisitiza Mabula.
No comments:
Post a Comment