Na Okuly Julius-Dodoma
Tafiti zinaonesha kuwa watu milioni 850 wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo duniani huku makadirio kwa watu waishio Kusini mwa jangwa la Sahara zinaonesha kuwa takriban watu 16 kati ya watu 100 wameathirika na tatizo hilo.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma kwa uratibu wa Chuo Kikuu cha Dodoma , leo Machi 14,2024, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Dkt. Caroline Damian amesema kuwa Nchini Tanzania, tafiti zinaonyesha kati ya asilimia 7% mpaka 14% ya watanzania ambayo ni wastani na watu 10 katika ya watu 100 wanaathiriwa na ugonjwa sugu wa figo.
“Wastani wa wagonjwa 9150 wenye matatizo ya figo yaliyopelekea figo zao kushindwa kufanya kazi wanahitaji huduma ya kusafisha damu (Haemodialysis) Hadi kufikia mwezi Desemba 2023, jumla ya wagonjwa 3231 wanapata huduma ya dialysis ikilinganisha na wagonjwa 1017 ambao walikuwa kwenye huduma hiyo mwezi Agosti 2019,
Na kuongeza kuwa “hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 68.5 ndani ya kipindi cha miaka minne. Mfuko wa bima ya Afya kwa sasa unabeba asilimia 80% ya gharama za wagonjwa walioko kwenye huduma ya uchujaji damu kwa sasa na mfuko unaelekea kuelemewa na mzigo huu,” ameeleza Dkt. Caroline
Amesema gharama za kukabiliana na ugonjwa huo ni kubwa hivyo Mgonjwa atahitaji kulipia wastani wa TZS. 1,320,000/= kwa ajili ya Vipimo kwa mwezi na gharama za huduma ya kusafisha damu (Hemodialysis) na wastani kati ya TZS. 31,200,000/= hadi 46,800,000/= kwa mwaka.
Katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa figo Dkt. Caroline amesema Wizara ya Afya imeendelea kutoa elimu ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo figo kupitia miongozo mbalimbali ikiwemo mwongozo wa mtindo bora wa maisha, lishe, mazoezi na taarifa ya hali ya matumizi ya tumbaku nchini. Vilevile, Wizara imeendelea na kampeni za kukinga na kutoa huduma za upimaji na utambuzi wa awali ili kudhibiti ongezeko la wananchi wenye magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo figo
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) , Mipango, Fedha na Utawala Profesa Wineaster Anderson amesema katika maadhimisho hayo, chuo hicho kitatoa huduma ya vipimo vya ugonjwa huo kwa siku tatu.
Amesema upimaji huo umeanza jana na utamalizika kesho na kwamba kwa siku mbili wamewaona na kuwapima watu 300 ugonjwa huo lengo likiwa ni kuwaona Wananchi wengi zaidi na zoezi hilo linafanyika bure katika viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma.
Siku ya figo Duniani huadhimishwa duniani kote kila alhamisi ya pili ya mwezi Machi kila mwaka tangu mwaka, 2006 na Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka 2024 ni “Afya ya Figo kwa wote, boresha usawa wa kufikia huduma na matumizi sahihi ya dawa ( kidney health for all- advancing equitable access to care and optimal medication practice)” Kauli mbiu hii imeandaliwa kwa kuzingatia hali halisi Duniani kote ambapo madhara yatokanayo na magonjwa ya figo yanaongezeka kwa kasi kubwa na kufanya huduma hizi kutolewa kwa wachache wanaomudu gharama. Wito ni kuzingatia kulinda afya za figo zetu kwa kuhakikisha unadhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza, kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya dawa na kutoa matibabu sahihi kwa wagonjwa wa figo.
No comments:
Post a Comment