UJENZI NA UBORESHAJI KIWANJA CHA NDEGE CHA TABORA KUKAMILIKA OKTOBA, 2024 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 13, 2024

UJENZI NA UBORESHAJI KIWANJA CHA NDEGE CHA TABORA KUKAMILIKA OKTOBA, 2024

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (wa kwanza kulia), akipokea maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb), wakati wakikagua utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora, Mkoani Tabora.
Mhandisi Alpha Nestory, akielezea mchoro wa jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Tabora kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati Wajumbe hao walipokagua utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja hicho Mkoani Tabora.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakati walipotembelea na kukagua utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora, Mkoani Tabora.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Doroth Mtenga akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora, kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani), Mkoani Tabora.
Kazi za ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora zikiendelea mkoani Tabora. Jengo hilo litakapokamilika litaweza kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja.

Na Mwandishi Wetu, Tabora 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa Serikali itahakikisha inasimamia ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora ili kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2024.

Bashungwa ameyasema hayo Machi 13, 2024 mkoani Tabora katika ziara ya Kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kusisitiza Wizara kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), itahakikisha inamsimamia Mkandarasi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG), kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa ubora.

"Mheshimiwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati, niwadhihirishie kuwa kutokana na baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika mradi, tutamsimamia Mkandarasi ili atukabidhi mradi mwezi Oktoba mwaka huu", amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa moja ya sababu ya miradi kuchelewa ni kutokana na Taasisi za Serikali kutoshirikiana kwa karibu katika maandalizi na utekelezaji wa mradi na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kushiriana na Makatibu wakuu wengine katika uratibu wa utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb) amemuagiza Waziri Bashungwa kuhakikisha anamsimamia Mkandarasi anayejenga na kukarabati Kiwanja cha Ndege cha Tabora kufanya kazi kwa ufanisi na ndani ya muda uliopangwa.
Kadhalika, Kakoso amemtaka Bashungwa kufuatilia upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi kwa wakati ili kuwawezesha Wakandarasi wanaotekeleza miradi nchini kupokea malipo yao kwa wakati yatakayofanikisha ukamilishaji wa miradi kulingana na mikataba.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Doroth Mtenga ameeleza kuwa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja hicho umefikia asilimia 38 na unahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja, ofisi mbalimbali, sehemu za biashara, ujenzi wa mnara wa kuongoza ndege na ujenzi wa barabara wa kuingia na kutoka kiwanjani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.

No comments:

Post a Comment