Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amesema kuwa kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Chanika – Mbagala Rangi Tatu kipande cha kilometa 3.8 kwa kiwango cha lami ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2024.
Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri huyo wakati akijibu Swali la Mbunge wa Mbagala, Mheshimiwa Abdallah Jafar Chaurembo, aliyehoji lini Serikali itamaliza ujenzi wa barabara kipande cha kilometa 5 kuanzia Mbande hadi Msongole.
Kasekenya ameeleza kuwa barabara ya Msongole – Mbande yenye urefu wa kilometa 7.4 ni sehemu ya barabara ya Chanika – Mbagala Rangi Tatu yenye urefu wa kilometa 29.20 ambapo kilometa 25.4 tayari zimeshajengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 3.8 zilizobaki ni changarawe.
“Ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu iliyobaki ya kilometa 3.8 ulianza mwezi Desemba, 2023 na kazi zimepangwa kukamilika mwezi Septemba, 2024”, amesema Kasekenya.
Kasekenya amemsisitiza Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha inapitika wakati wote hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zinaendelea kunyesha katika jiji la Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment