KAMISHNA JENERALI wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam |
Picha mbalimbali zinazoonesha jumla ya kilogramu 353.52 za dawa za kulevya zilizokamatwa kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam. |
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni na kufanikiwa kukamata jumla ya kilo 767.2 za dawa za kulevya katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Aprili 4 hadi 18, 2024.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ametangaza mafanikio hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 22 Aprili, 2024, jijini Dar es Salaam na kusema kuwa, aina ya dawa zilizokamatwa ni pamoja na heroin (kilo 233.2), methamphetamini (kilo 525.67) na skanka (kilo 8.33) ambapo watu 21 wamekamtwa.
"Watuhumiwa 21 wamekamatwa kuhusiana na dawa za kulevya zilizokamatwa, baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa taratibu za kisheria zitakapokamilika" amesema Lyimo
Amezitaja operesheni zilizofanikisha ukamataji wa dawa hizo kuwa ni ilizofanyika jijini Tanga eneo la Mikanjuni tarehe 4 Aprili,2024 ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa na gramu 329.412 za heroin, iliyofanyika eneo la Wailes Temeke mtaa wa Jeshini jijini Dar es Salaam tarehe 8 Aprili, 2024 na kufanikisha watuhumiwa wawili kukamatwa na kilogramu 1.49 za skanka, iliyofanyika eneo la Zinga Bagamoyo mkoani Pwani tarehe 10 Aprili, 2024 na kufanikisha kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na kilogramu 424.84 za dawa ya kulevya aina ya Methamphetamine. Pia mtuhumiwa mwingine mmoja alikamatwa na gramu 158.24 za heroin eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili.
"Aidha, tarehe 14 Aprili, 2024 tulifanya operesheni katika eneo la bandari jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata kilogramu 4.72 za dawa za kulevya aina ya skanka pamoja na kuwakamata watuhumiwa watatu kuhusika na dawa hizo.
Vilevile, tarehe 16 Aprili, 2024 tuliendelea na operesheni jijini Dar es Salaam, katika kata ya Kunduchi na kukamata kilogramu 232.69 za dawa za kulevya aina ya heroin na kilogramu 100.83 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi. Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni tisa" amesema Lyimo.
Ameendelea kusema kuwa, mtuhumiwa mmoja alikamatwa tarehe 18 Aprili eneo la bandari jijini Dar es Salaam akiwa na kilogramu 2.12 za skanka.
Pia amefichua mbinu mpya ya ufichaji wa dawa za kulevya inayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha dawa hizo haramu. Ameeleza kuwa baadhi ya dawa zilizokamatwa zilikuwa zimefichwa kwa ustadi kwenye vifungashio vilivyoandikwa majina ya kahawa na chai ili kukwepa kukamatwa.
Akiangazia tishio la dawa za kulevya linalokua kwa kasi duniani, Kamishna Lyimo ametoa wito kwa jamii kuungana katika kupambana na janga la dawa za kulevya kwani vijana ni kundi linaloathirika zaidi.
"Vijana ni nguvu kazi ya Taifa letu. Kama wakiendelea kuathiriwa na dawa za kulevya, uchumi na usalama wa nchi vitakuwa hatarini. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kupambana na janga hili. Tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili kulinda taifa letu dhidi ya janga hili kwa kupiga namba yetu ya bure 119” amesema Lyimo.
Kamishna Jenerali Lyimo ametoa shukrani kwa wadau wote wanaoshirikiana na DCEA katika vita dhidi ya dawa za kulevya, hasa vyombo vya ulinzi na usalama na kuahidi kuwa DCEA itaendelea kupambana ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi salama na isiyo na dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment